1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Monaco ina kibarua kigumu dhidi ya Juve

Sekione Kitojo
9 Mei 2017

Ni timu zipi zitaelekea Cardiff kwa fainali ya Champions League barani Ulaya, swali  hilo linaanza kupatiwa jibu leo wakati  mkondo wa pili wa mchezo wa nusu fainali kati ya Juventus, na AS Monaco utakapofanyika.

https://p.dw.com/p/2ch3K
UEFA Champions League Halbfinale AS Monaco - Juventus
Washambuliaji hatari wa AS Monaco Kylian Mbappe na Radamel Falcao Picha: picture-alliance/Zumapress/M. Ciambelli

Monaco  pamoja  na  Atletico  Madrid  zinakabiliwa  na  majukumu ambayo  yanaonekana  kuwa  karibu  ya  kutowezekana  katikati  ya wiki  hii  katika  michezo  ya  mkondo  wa  pili wa  nusu  fainali  ya kombe  la  ligi  ya  mabingwa ,  Champions League  barani  Ulaya, ambapo  wapinzani  wao  Juventus  na  Real Madrid  wapo  katika ukingo wa  kukutana  mjini  Cardiff  katika  fainali  ya  mwaka  huu 2017.

Fußball AS Monaco v Juventus Turin - UEFA Champions League Juventus' Gonzalo Higuain celebrates scoring their second goal with Miralem Pjanic
Gonzalo Higuain akikumbatiwa na mchezaji mwenzake Miralem Pyanic baada ya kufunga baoPicha: Reuters/E. Gaillard

Hata  kocha  wa  Monaco Leonardo  Jardim  anaukadiria  mchezo huo  kwa  kiwango  cha  nafasi  moja  tu  katika  20 zilizopo. Na wengi  wangesema  kwamba huo ni  msimamo wa  matumaini  kwa nafasi  ilizonazo  kikosi  chache  chenye  wachezaji  wachanga kuweza  kubadilisha  matokeo  ya  awali  ya  mabao 2-0 dhidi  ya Juventus  Turin.

Mabingwa  hao  watarajiwa  wa  ligi  ya  Ufaransa  ambao  hupachika mabao  bila  shida  katika  ligi  ya  nyumbani , wamepachika  mabao 3 mara  27  msimu  huu. Lakini  hakuna  timu  iliyokwisha  fanya hivyo  dhidi  ya  ngome  ya  Juventus  ambayo  imeruhusu  mabo mawili , mara  tano  tu  katika  michezo  51  katika  kampeni  ya mwaka  huu, haijashindwa  nyumbani  katika  muda  wa  miezi 20  na ngome  yake  imevujisha  mabao  mawili  tu  katika  michezo  11  ya Champions League.

Fußball AS Monaco v Juventus Turin - UEFA Champions League
Mpambano kati ya Monaco na Juventus Turin wa nusu fainali mjini MonacoPicha: Reuters/E. Gaillard

Takwimu  hizi  zinatoa  nguvu  zaidi  kwa  Bibi Kizee, wakati  timu hiyo  ikiwa  na  uwezo  wake  wote  wa  wachezaji, kama  ilivyokuwa wakati  walipofanikiwa  kutuliza  mzuka  wa  washambuliaji  hatari  wa Monaco  katika  mji wa  kitalii  wa  Monaco wiki  iliyopita, ama wakati  Leo Messi  na  wenzake   wa  Barcelona walipopigwa sindano  ya  ganzi  na  kuendeshwa  mchakamchaka  mjini  Turin.

Kutokana  na  hilo, kocha  wa  Monaco Jardim  alisema  jukumu  lake la  kwanza  lilikuwa  kuingiza  imani  katika  kikosi  chake kwamba hawapambani  na  dude lililokufa.

"ni  wajibu  wetu  kufanya  kitu  tofauti. Iwapo unashindwa  nyumbani kwa   mabao 2-0 ni  wazi kwamba  unapaswa  kuja  na  kitu cha ziada," Jardim  alisema  katika  mkesha  wa  kuamkia  mchezo  huo.

"Mjini  Monaco  tulipata  kipigo kutokana  na uzoefu: mikwaju yetu kuelekea  golini  ilikuwa  sawa  na  Juventus. Tofauti  ilikuwa kiwango  cha  mafanikio  yao  kilikuwa  asilimia  100, kwa  upande wetu  ilikuwa  ziro."  Ameongeza  Jardim.

Inter Mailand AC Mailand 2010
Kocha wa Juve Massimiliano AllegriPicha: AP

Kocha  wa  Juve Massimiliano Allegri  alicheka  baada  ya kuambiwa  kwamba  matokeo yamekamilika  na  timu  yake  tayari  ni mshindi. "Huwezi  kujua  kile  kitakachotokea  katika  mchezo. Monaco huenda  wakaingia  katika  mchezo  huo  katika  mtindo tofauti kabisa na  kufanya  hali  kuwa  ngumu na  wana  wachezaji wenye  uwezo  mkubwa, vipaji  vya  juu  kabisa," amesema.

"Tunapaswa  kuanza  mwanzo  kabisa , tuhakikishe  tunacheza  kwa nguvu  katika  mchezo  huo  na  matumaini  ni  kwamba  tutakuwa bora  kiufundi  kuliko  tulivyokuwa  kule  Monaco, ambako  tulipata fursa  nyingi  na  kutengeneza  mazingira  yaliyoleta  hatari na  mara nyingi  tulifanya  makosa.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / afpe / dpae

Mhariri: Iddi Ssessanga