MONUSCO huenda ikasimamia chaguzi za Congo
21 Machi 2018Rasimu hiyo iliyoandikwa na Ufaransa itaongeza muda wa kuhudumu kwa kikosi cha MONUSCO kwa mwaka mmoja zaidi na kubainisha vipaumbele ambavyo kikosi hicho vitashughulikia Congo inayoelekea katika uchaguzi mkuu tarehe 23 Desemba mwaka huu.
Chaguzi hizo katika taifa hilo lenye utajiri wa madini na mali asili zinatarajiwa kumchagua kiongozi mpya atakayemrithi Rais Joseph Kabila aliyeingia madarakani mwaka 2001 baada ya baba yake kuuawa akiwa madarakani. Kabila ambaye amekatalia madarakani hajatangaza wazi kama tawania au la katika uchaguzi huo.
Rasimu hiyo iliyowasilishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linataka MONUSCO kuwalinda raia, kushiriki katika mchakato wa uchaguzi, ikiwemo kusajili wapiga kura, kuuandaa uchaguzi na kusimamia shughuli za kukabidhi madaraka mnamo tarehe 12 Januari.
Baraza hilo litapigia kura rasimu hiyo tarehe 27 mwezi huu na wanadiplomasia wanatarajiwa litaungwa mkono na wanachama wa baraza hilo.
Umoja wa Mataifa kushika usukani
Iwapo rasimu hiyo ya azimio kuhusu Congo itapitishwa, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ataombwa kufanya mipango ya kukiimarisha kikosi hicho cha MONUSCO.
Atatakiwa kuripoti mipango aliyoichukua kuhakikisha MONUSCO ina uwezo wa kutosha kusimamia chaguzi Congo katika kipindi cha siku tisini baada ya kupitishwa kwa azimio hilo.
Mwaka jana kufuatia shinikizo kutoka kwa Marekani, Baraza hilo la Usalama lilipunguza idadi ya wanajeshi wanaohudumu chini ya ujumbe wa MONUSCO kwa kuwaondoa wanajeshi 3,600 na kuwaacha wanajeshi 16,215 pamoja na polisi 1,450 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.
Licha ya punguzo hilo, kikosi cha MONUSCO kinasalia kikubwa zaidi cha wanajeshi wa kulinda amani Umoja wa Mataifa.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Congo Leila Zerrougi ameonya kuwa huenda kukazuka ghasia nchini humo kuelekea uchaguzi akiilaumu serikali ya Rais Joseph Kabila kwa kushindwa kuheshimu makubaliano ya kisiasa, kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na kutoheshimu haki ya kuandamana.
Nchi hiyo imeshuhudia misururu ya maandamano tangu mwaka jana ya kumshinikiza Rais Kabila kuachia madaraka. Muhula wake wa pili madarakani ulikamalika mwezi Desemba mwaka 2016.
Makubaliano kati ya serikali na upinzani yaliyosimamiwa na Kanisa Katoliki, yalimpa ridhaa ya kusalia madarakani hadi mwishoni mwa mwaka jana, ambapo chaguzi zilipaswa kuandaliwa mwezi Desemba lakini hazikufanyika baada ya tume ya uchaguzi kusema haikuwa tayari kuandaa chaguzi hizo kutokana na changamoto za kiufundi.
Guterres anapanga kufanya ziara katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo akiandamana na Rais wa halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat katika miezi michache ijayo kutathimini hali ya kisiasa na kiusalama nchini inayoutia jumuiya ya kimataifa wasiwasi kuelekea uchaguzi.
Mwandishi: Caro Robi/Afp
Mhariri: Daniel Gakuba