Moto Urusi wafika kwenye mkoa wa Bryansk
11 Agosti 2010Shirika la taifa la kuhifadhi misitu nchini Urusi limethibitisha kuwa moto wa misituni unaondelea kuwaka nchini humo umeyafikia maeneo yaliyoathiriwa na ajali iliyotokea kwenye kinu cha kinyuklia huko Chernobyl. Moto huo unaelezwa kuufikia mkoa wa Bryansk ambao umeathiriwa na miale yenye sumu iliyotokana na maafa kwenye kinu hicho.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Agosti 6 na shirika la taifa la kuhifadhi misitu nchini Urusi la Roslesozaschita, visa 28 vya moto vimeripotiwa katika mkoa wa Bryansk wenye jumla ya hekta 269. Mkoa huo uliopo magharibi mwa Urusi uliathiriwa na ajali hiyo ya kinu cha kinyuklia cha Chernobyl mwaka 1986. Mapema wiki hii maafisa wa wizara ya masuala ya dharura walikanusha kuwa moto umesambaa katika mkoa huo, baada ya kuzuka wasi wasi kuhusu chembe chembe za nyuklia zilizopeperushwa hewani kutoka kwenye mchanga na moto huo. Shirika hilo limesema kuna ramani ambazo zinaonyesha maeneo yaliyoathiriwa na miale hiyo yenye sumu na kuna ramani zinazoonyesha moto.
Katika taarifa iliyotoa kwenye mtandao wake, shirika hilo limesema kuwa kiasi hekta 3,900 za ardhi ya Urusi zinazoaminika kuwa na vimelea hivyo vyenye sumu zimeathiriwa na moto huo wa misituni. Wizara hiyo inayoshughulika na masuala ya dharura nchini Urusi imesema kuwa vikosi zaidi vya kuzima moto vimesambazwa kuzuia moto katika maeneo hayo. Vikosi hivyo pia vilipambana kuuzuia moto usifike katika kiwanda kikuu cha kusafisha taka za kinyuklia kilichopo Ozersk katika eneo la Urals. Wakati huo huo, watabiri wa hali ya hewa wamesema kuwa hali ya joto kali kuzunguka Urusi iliyosababisha moto kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hiyo inaweza kuendelea kwa muda wa siku kumi zaidi.
Aidha, viwango vya uchafuzi wa hali ya hewa vimeongezeka mjini Moscow, hivyo kusababisha wakaazi wengi wa mji huo kuukimbia moshi mkubwa uliotanda. Maafisa pia wamesema mbali na vikosi vya zima moto, watu kadhaa wanapambana na moto huo kwenye maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Katika hatua nyingine, zao la ngano kwa mwaka huu limeharibiwa kutokana na hali hiyo mbaya ya hewa. Urusi ambayo ni nchi ya tatu kwa kulima ngano na kusafirisha zao hilo nje ya nchi, imelazimika kupiga marufuku kusafirisha nje zao hilo kutokana na janga hilo. Hatua hiyo imesababisha bei za ngano duniani kupanda.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFPE)
Mhariri:Othman Miraji