Mradi wa vipindi vya Noa Bongo Jenga Maisha Yako washinda tuzo
28 Septemba 2010Mradi wa Learning by Ear - Noa Bongo Jenga Maisha Yako umeshinda tuzo ya mashindano ya maeneo 365 nchini Ujerumani yanayovumbua mawazo mapya. Mkurugenzi wa benki ya Ujerumani ya Deutsche Bank mjini Cologne, Thomas Illemann, alimkabidhi tuzo hiyo Mkurugenzi mtendaji wa shirikala la utangazaji la Deutsche Welle mjini Bonn, Erik Betterrmann, katika hafla iliyofanyika hapa hapa katika ofisi za DW mjini Bonn siku ya Alhamisi iliyopita. (23.09.2010)
Mradi wa Learning by Ear "Noa bongo jenga maisha yako" unakuwa sasa moja wapo ya maeneo nchini Ujerumani, ambayo huchaguliwa kila mwaka, kama maeneo ya kuvumbua mawazo mapya na kutunzwa na benki ya Ujerumani ya Deutsche Bank chini ya mwavuli wa ofisi ya Rais wa Ujerumani.
Wakati wa kutolewa kwa tuzo hiyo, mkurugenzi wa benki ya Deutsche Bank, Thomas Illemann, alisema Deutsche Welle imepiga hatua kubwa katika masuala ya utangazaji kupitia mradi wa Noa Bongo Jenga Maisha Yako chini ya kauli mbiu "Sikiliza na uboreshe maisha yako ya siku za usoni."
Vipindi vya Noa bongo Jenga maisha yako, vinaangalia changamoto ambazo anakabiliana nazo kijana wa Kiafrika na vinawaweka karibu wasikilizaji katika njia ya kupata taarifa pamoja na burudani. Vipindi hivi ni mchanganyiko wa ripoti, michezo ya redio pamoja na taarifa za makala ambazo zinampa msikilizaji nafasi ya kupata mbinu muhimu za kuweza kufanikiwa katika maisha yake.
Mkurugenzi wa idara za Afrika na Mashariki ya Kati, Bi Ute Schaeffer, aliyeuanzisha mradi wa Noa Bongo, alisema anajivunia mradi huo kushinda tuzo ya uvumbuzi wa mawazo mapya. Aliongeza kuwa tuzo hiyo inampa ari mpya ya kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na kuuendeleza mradi huo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Deutsche Welle, Erik Betterman alisema uamuzi wa jopo maalumu la majaji kuupa tuzo hiyo mradi wa Learning by Ear, Noa Bongo Jenga Maisha Yako, umeifanya Deutsche Welle, kujivunia kazi yake ya mradi huo.
Halima Nyanza alihudhuria hafla hiyo iliyoandaliwa katika ukumbi wa Gremiensaal hapa Deutsche Welle na kuzungumza na Crispin Mwakideu, mmoja wa waandishi wa michezo ya redio ya mradi wa Noa Bongo Jenga Maisha Yako na Maja Dreyer anayeratibu mradi mzima.
Mwandishi: Halima Nyanza
Mhariri: Josephat Charo