Mshukiwa janga la moto mjini Paris akamatwa.
5 Februari 2019Picha za vidio kutoka eneo la tukio zimeonesha moshi mkubwa ukifuka kutoka madirisha ya ghorofa la juu ya jumba hilo wakati vikosi vya waokoaji vikijaribu kuwaokoa wahanga walio kwenye taharuki ambao baadhi walikiwa wamevalia mavazi ya kulalia pekee.
Kiasi wazima moto 200 na zaidi gari 100 za kuzima moto zilitumika kwa muda saa tano kujaribu kuudhibiti moto huo uliozuka majira ya saa saba usiku saa za Ufaransa.
Tukio hilo la moto juu ya jumba hilo la ghorofa katika eneo la kusini magharibi ya mji wa Paris ndiyo baya zaidi kutokea tangu mnamo mwaka 2005 wakati watu 24 walipoteza maisha kwa janga la moto kwenye hoteli moja katikati ya mji huo mkuu wa Ufaransa.
Taharuki ilikuwa kubwa
Idara ya kukabiliana na majanga ya moto imesema zoezi la ukoaji kwenye mkasa huo lilikuwa gumu na la kutisha ambapo watu kumi wamekufa ikiwemo wazimamoto 6 na kuwaacha zaidi ya watu wengine 30 wakiwa wamejeruhiwa.
Walioshuhudia mkasa huo wamesema tukio hilo lilikuwa la kuhuzunisha na shughuli za uokozi zilitatizwa na kiwango kikubwa cha moto na hali ya taharuki iliyozuka.
Shuhuda mmoja wa mkasa huo alisema "Tangu mwanzo kulikuwa na watu wakipiga yowe, watu walikuwa tayari kwenye kuta wakijaribu kutoka kwa kuteleza pembezoni mwa roshani. Na wakati huo kikosi cha kuzima moto kilikuwa ndo kwanza kinakaribia ghorofa ya pili na walikuwa wakipata tabu kufikia kila ghorofa kwa kutumia ngazi. Nikajisemea hakuna tena muda wa kutosha.”
Rais wa Ufaransa Emanuel Macron ametuma salamu za pole na rambirambi kupitia ukurasa wake wa twitter na kuutaja mkasa huo kuwa huzuni kwa wakaazi wa Paris na raia wa Ufaransa.
Siyo shambulio la kigaidi.
Mwendesha mashatka mkuu wa mjini Paris Remy Heitz amesema akiwa katika eneo la tukio kuwa mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 40 aliye na historia ya matatizo ya akili amekatwa kuhusiana na mkasa huo.
Kukamatwa kwake kumeondoa hofu ya hapo kabla kuwa huenda tukio la moto huo lilikuwa la kigaidi.
Uchunguzi umeanzishwa wa kosa la jinai la kujaribu kuua kwa kutumia moto wakati wasiwasi unaongezeka kuwa idadi ya watu waliokufa huenda ikapanda pindi polisi itakamilisha upekuzi katika ghorofa zilizoteketea.
Mkasa huo wa siku ya Jumanne umetokea kiasi mwezi mmoja tangu mripuko ulisababishwa na kuvuja kwa gesi katika duka la kuuza mikate mjini Paris kusababisha moto uliowaua watu wanne.
Mwandishi: Rashid Chilumba/AP/AFP
Mhariri: Josephat Charo