1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtoto wa rais wa zamani wa Gabon ashinda uchaguzi wa rais

Oumilkher Hamidou3 Septemba 2009

Upande wa upinzani wayakataa matokeo ya uchaguzi nchini Gabon

https://p.dw.com/p/JOY5
Rais mpya wa Gabon Ali BongoPicha: picture-alliance/ dpa

Ali Bongo,mtoto wa kiume wa rais aliyefariki dunia wa nchi hiyo tajiri ya Afrika Magharibi,Omar Bongo Ondimba,ametangazwa kua mshindi wa uchaguzi wa rais-matokeo ambayo yanabishwa na upande wa upinzani.Machafuko yameripotiwa mara baada ya matokeo hayo kutangazwa.

Ali Bongo,mwenye umri wa miaka 50 ameshinda kwa asili mia 41.73 dhidi ya 25.88 za mpinzani wake,waziri wa zamani wa mambo ya ndani André Mba Obame na mgombea wa kujitegemea,Pierre Mamboundou aliyejikingia asili mia 25.22 ya kura.

Katika hotuba yake mara baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa,,matokeo ambayo wapinzani wake wawili wakuu walijitangazia ushindi tangu siku kadhaa zilizopita,Ali Bongo ameahidi kuwa "rais wa wananchi wote wa Gabon".

Ali Bongo anasema:

"Ni muhimu kwetu kuimarisha urithi wetu."

Ali Bongo ameahidi kuheshimu ahadi alizotoa wakati wa kampeni ya uchaguzi,ikiwa ni pamoja na "kufuata nyayo za mtanagulizi wake,kuleta mageuzi yanayohitajika,kuimarisha maendeleo,kuimarisha bajeti na kuleta hali ya haki na usawa."

Lakini mshauri wa André Mba Obame amesema hawayatambui matokeo hayo na kushadidia mgombea wao yuko "mahala salama na pa siri."

Mpinzani mashuhuri wa Gabon Pierre Mamboundou,aliyeungwa mkono katika uchaguzi huo wa Agosti 30 iliyopita na vyama vitano vya kisiasa nae pia ameingia mafichoni.Wafuasi wake wanasema wanajiandaa kutoa taarifa .

Matokeo ya uchaguzi yalikua yatangazwe jana usiku,lakini matatizo ya kiufundi ya halmashauri huru na ya kudumu ya uchaguzi-Cénap yamepelekea kukawilishwa.

Katika wakati ambapo matokeo hayo ya uchaguzi yalikua yakitangazwa jimbo moja moja,leo asubuhi wafuasi wa kiongozi wa upinzani Pierre Mamboundou waliivamia jela ya Port-Gentil -mji wa pili muhimu wa nchi hiyo.

Wamewaachia huru wafungwa na baadae kuongozana hadi eneo la kati la mji huo ambako vizuwizi viliwekwa majiani.Kwa mujibu wa ripota wa shirika la habari la Ufaransa AFP jengo moja lilikua linawaka moto.

Muda mfupi baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa,ubalozi mdogo wa Ufaransa mjini Port-Gentil ukatiwa moto na wafuasi wa upande wa upinzani.

Frankreich Neues Kabinett Bernard Kouchner
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Bernard KouchnerPicha: AP

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Bernard Kouchner amehakikisha "nchi yake ina mpango wa kuwalinda raia zake nchini Gabon."Inakadiriwa wafaransa elfu kumi wanaishi nchini Gabon.

Upande wa upinzani unaituhumu Ufaransa,mkoloni wa zamani wa Gabon kumuunga mkono Ali Bongo.

Machafuko yameripoti pia katika mitaa kadhaa ya mji mkuu Libreville ambako maripota wa shirika la habari la Ufaransa AFP wanasema magari yalitiwa moto ,madebe ya taka yamepinduliwa,maduka yameporwa na masamu kuvunjwa majiani.

Vikosi vya usalama viliingilia kati na kuwatawanya waandamanaji,miongoni mwao walikuwemo pia wagombea walioshindwa,André Mba Obame na Pierre Manboundou.

"Jeshi limefyetua risasi na kuvurumisha maguruneti amesema mshauri mmoja wa Mamboundou aliyeongeza kusema bwana Mamboundou amejeruhiwa "kichwani na begani".Hali yake inasemekana ni mbaya.

Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/AFP

Mhariri M.Abdul-Rahman