MUMBAI: Mafuriko yalikumba jimbo la Maharashtra nchini India
1 Agosti 2005Maofisa wa serikali katika jimbo lililokumbwa na mafuruko la Maharashtra nchini India, wamewaonya raia kubakia nyumbani kufuatia mvua kubwa iliyonyesha mjini Mumbai na vitongoji vyake. Mvua hiyo imetatiza juhudi za usafishaji na kuwapelekea chakula waathiriwa wa mafuriko hayo.
Siku tano baada ya mvua kubwa kunyesha magharibi mwa India, wanajeshi, maofisa wa ulinzi na watoa misaada ya kiutu wameendelea na juhudi zao za kuzisaka maiti za watu waliouwawa na mafuriko katika wilaya zilizoathiriwa zaidi. Watabiri wa hali ya hewa wamesema mvua kubwa zaidi inatarajiwa kunyesha katika kipindi cha saa 48 zijazo.
Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, ametoa msaada wa kitaifa kwa jimbo hilo la Maharashtra. Polisi wanasema watu yapata 1,000 wamefariki dunia kufuatia mafuriko na maporomoko ya ardhi tangu Jumatatu iliyopita.