1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano juu ya Korea ya Kaskazini

15 Februari 2005

Tamko la Korea ya kaskazini kwamba ina silaha za nyuklia ili kujihami dhidi ya mashambilizi ya Marekani limeifadhaisha China. Tamko hilo linafichua msimamo nduma kuwili wa nchi hiyo yaani China juu ya Umoja wa Mataifa inapohusu suala la Korea ya kaskazini.

https://p.dw.com/p/CEGP

China ni muhimu sana katika kutatua mzozo juu ya nchi hiyo unaotokana na kumiliki silaha za nyuklia.

Tokea Korea iwafukuze nchini,wawakilishi wa shirika la kimataifa linaloshughulikia nishati ya nyuklia, China imekuwa inakinza juhudi zote,kwenye baraza la usalama zenye lengo la kuirudi Korea.

Badala yake China imeamua kuwa msuluhishi wa suala la nykulia la Korea

kwa kuandaa mazungumzo baina yake na Marekani,Korea zote mbili na Japan.

Hatahivyo mazungumzo ya hapo awali juu ya suala hilo hayakuzaa matunda yoyote.

Korea iliifanya jumuiya ya kimataifa ipigwe butaa ilipotangaza kujitoa kwenye mazungumzo ya kutatua mzozo wa silaha za nyuklia .Viongozi wa nchi hiyo wamesema wanaendelea na mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia kwa lengo la kulinda itikadi,uhuru na demokrasi iliyochaguliwa na wananchi.

Mtafiti wa masuala ya kimataifa kwenye taasisi ya sayansi za jamii nchini China bwana Shen Jiru amesema hali itakuwa ngumu ikiwa kama Marekani itapeleka shauri la Korea mbele ya Umoja wa Mataifa.

Hadi sasa China imekuwa inapinga msimamo wa Marekani wa kujaribu kutatua mgogoro wa Korea peke yake,

na imekuwa inaunga mkono haja ya baraza la usalama kuhusika katika mazungumzo.

Katika kutetea siasa ya kutojiingiza katika mambo ya ndani ya nchi nyingine, viongozi wa China wamehoji kwamba nguvu za kijeshi asilani zisitumiwe katika kutatua mizozo ya kimataifa .

Hatahivyo China wakati wote imekuwa inasimama kidete katika kupinga juhudi za baraza la usalama za kuiwekea vikwazo Korea ya Kaskazini

licha ya ukweli kwamba nchi hiyo

inakiuka sheria za kimataifa.

Mnamo mwaka wa 2003 Korea ya Kaskazini ilijitoa kwenye mkataba juu ya kutoeneza silaha za nyuklia na iliamua kuwafukuza wakaguzi wa kimataifa baada ya ushahidi kuonyesha kwamba nchi hiyo ilikuwa na mpango wa kurutubisha madini yaUraniaum.

Sasa Korea imekiri rasmi kwamba ina silaha za nyuklia baada ya kukanusha jambo hilo kwa muda mrefu.

Lakini China ,rafiki na ndugu,kiitikadi na Korea za Kaskazini haijatoa sauti ya juu ,juu ya hatari hiyo. Vyombo vya habari vya nchi hiyo pia vinazungumza kwa sauti ya chini.

Hatahivyo gazeti la Beijing News limesema kwamba tangazo rasmi la Korea kwamba ina silaha za nyuklia lina lengo la kuvutia makini ya jumuiya ya kimataifa ili kuweza kupata misaada zaidi ya maendeleo.

Waziri wa mambo ya nje wa China amemwahidi waziri mwenzake wa Marekani bibi Condoleeza Rice kwamba nchi yake itafanya kila linalopasa ili kuishawishi Korea ya Kaskazini irejee kwenye mazungumzo.

Waziri huyo wa China bwana Li amesema nchi yake inaunga mkono sera ya kuhakikisha kwamba eneo la lote la Korea linakuwa huru na silaha za nyuklia.

Wakati huo huo Marekani imeendelea kudai kwamba viwanda vya silaha vya serikali ya China vimesaidia katika mpango wa nyuklia wa Korea

Wataalamu wanaamini kwamba Korea ya Kaskazini tayari ina mabomu kumi ya atomiki.Na kama madai hayo yatathibiti kuwa ya kweli pana mawezekano ya nchi kama Korea ya Kusini na Japan pia kuanzisha mipango ya kuunda silaha za nyuklia.