Mwaka mmoja wa COVID-19 barani Afrika
11 Machi 2021Moja ya matokeo mabaya kabisa ya janga hili la COVID-19 ni kusababisha matatizo ya muda mrefu kiuchumi. Tangu hapo barani Afrika, uchumi ulishaathirika kutokana na vikwazo vya kibiashara na kuporomoka kwa mahitaji ya bidhaa duniani, na sasa ufungwaji mipaka ulizidi kuiuwa kabisa sekta ya utalii na sekta isiyo rasmi.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, ukuwaji wa uchumi kwa mataifa ya Afrika yaliyo kusini mwa jangwa la Sahara ulisinyaa kwa wastani wa asilimia 3.7 mwaka jana.
"Kwa mujibu wa ripoti hii, kutakuwa na anguko la asilimia 20 kwenye pato la kifamilia, ambayo itamaanisha kuwa zaidi ya watu milioni 400 duniani watashuka hadi mstari wa mwisho wa ufukara kwa pato la dola moja na senti tisiini kwa siku. Zaidi ya robo ya watu hao wanaishi Afrika iliyo kusini mwa jangwa la Sahara." Alisema Anja Osterhaus wa shirika la misaada la Oxfam kwenye mazungumzo yake na DW, akisisitiza kwamba utafiti wao unaonesha kuwa vita dhidi ya virusi vya corona vitaurudisha uchumi wa Afrika miaka 30 nyuma.
Athari kwa familia na wasichana
Lakini haukuwa uchumi pekee ulioathirika, bali pia maisha na afya za watu. Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), wanawake na watoto ni waathirika wakubwa zaidi wa athari za janga hili, kwani familia masikini zimejikuta zikibeba machungu makubwa zaidi ya kile kilichopotea kwenye kipindi cha vita vya corona.
"Nchini Afrika Kusini, ambako kama ilivyo kwengine skuli zilifungwa, kiasi cha watoto milioni 30 waliathirika. Iwe wale wa skuli za serikali ama za binafsi. COVID-19 ilikuja kuongezea matatizo ya ukosefu wa usawa ambayo tayari yalishakuwepo. Wanafunzi masikini walikuwa na fursa chache ama hawakuwa nazo kabisa katika kujifunza kupitia mtandao, huku wa kitajiri wakiwa na fursa hizo peke yao," anasema Andile Dube wa UNICEF.
Kuna watoto kadhaa wa kike ambao kufungiwa ndani kuihofia corona, kulimaanisha kubakwa na wengine kuolewa wakiwa wadogo, na kwenye maeneo mengi hawaruhusiwi kurejea tena masomoni hata hapo watakapokuwa wamejifunguwa.
Hata hivyo, kuna upande mwengine wa janga hili ambao umeleta neema barani Afrika, nao ni kuja juu kwa biashara ya mtandaoni. Kwa mujibu wa Nicholas Kendall wa kampuni ya GreenTec Capital inayojihusisha na kampuni changa changa barani Afrika, "idadi ya kampuni hizo na mikataba ya kibiashara imeongezeka barani humo licha yam waka 2020 kuwa mwaka mgumu kutokana na COVID-19."