Mwandishi wa Rwanda, Mbaroni Burundi
12 Juni 2015Taarifa hiyo imetolewa Juni 10 na kituo cha radio cha kimataifa cha Ufaransa RFI.
Mkurugenzi wa Raidio Izuba, Aimable Rwigamba, amethibitisha kukamatwa kwa Etienne Besabesa, ambae pia amekuwa akifanya kazi kama mwandishi wa kujitegemea katika shirika lake binafsi la habari la Igihe media group.
Mkurugenzi huyo ameonesha kwamba mpaka sasa sababu za kukamatwa kwa mwandishi huyo hazijaweza kufahamika. Kwa mujibu wa Rwigamba, mwandishi huyo alipewa jukumu la kwenda kuripoti katika eneo la Gihara, katika wilaya ya Kirege kusini/mashariki mwa Rwanda, ambayo inapakana na mji wa Muyinga wa Burundi. Imeripotiwa alivuka mpaka na kuingia Burundi wakati alipokamatwa.
Kukamatwa kwa Etienne
Lakini duru nyingine zinaeleza mwandishi huyo alikamatwa wakati akiwa katika jitihada za kuandika habari kuhusu wimbi la wakimbizi kutoka Burundi na kuingia Rwanda. Tayari kwa upande wake Kamisheni ya vyombo vya habari ya Rwanda RMC imetoa wito kwa serikali ya Burundi kumwachia huru mwandishi huyo.
Wakati hayo yanatokea, radio nchini Burundi zimesalia pasipo matangazo huku serikali ikiliweka katika kibano zaidi shirika la utangazaji la taifa.
Taarifa ya shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka inasema vituo vikubwa vya kibinafsi vya radio na televisheni sio tu kwamba vimeendelea kulazimishwa kufungwa lakini pia vimepigwa marufuku kutumia studio ya pamoja iliyopo mjini Bujumbura inayoitwa House of Presse, ambayo iliruhusiwa kurejesha upya shughuli za vyombo hivyo.
Hatma ya vyombo vya habari
Katika barua yake kwa kiongozi wa studio hiyo, mwendesha mashitaka wa serikali Valentin Bagorikunda ametoa ruhusa ya kufunguliwa tena kwa studio hiyo ambayo umoja wa watangazaji umekuwa ukiitumia mpaka kufungwa kwake Aprili 27 mwaka huu.
Lakini kumekuwa na vikwanzo. Barua ya Bagorikunda inasema kutokana na uchunguzi wa kimahakama mwajiriwa yeyote wa radio Bonesha FM, Radio Television Renaissance, Radio RPA( Bujumbura na Ngozi) Radio Isanganiro na Radio Humuriza FM ni marufuku kutumia studio hiyo.
Kwa hali iliyo wazi kabisa utekelezaji wa amri hiyo unamweka kando kabisa na jukumu la habari mwandishi yeyote anaefanya kazi katika kituo cha radio au televisheni isipokuwa tu, Radio Rema, ambayo nayo ipo katika uchunguzi wa kimahakama lakini vilevile inatajwa kuiunga mkono serikali.
Serikali ya Burundi vilevile inaelezwa kuongeza mbinyo kwa radio ya taifa nchini humo ambayo mpaka katika siku za hivi karibuni ilikuwa ikitimiza wajibu wake kwa ufasaha, ambapo wakati mwingine ilikuwa ikiwahoji wapinzani wa serikali na kutangaza hata maandamano yaliyokuwa yakiendelea nchini humo. Mkuu wa radio hiyo Freddy Nzeyimana alifukuzwa kazi Juni 4 na nafasi yake kuzibwa na Jouma Leonard Dwayio, mwalimu wa shule ya msingi.
Baadhi ya waandishi habari wa wanaofanya kazi na mashirika ya kimataifa wameliambia shirika la waandishi wa habari wasio na mipaka kwamba wamekuwa wakifanyiwa unyanyasaji, au kutishiwa usalama na vikosi vya usalama jambo ambalo limesababisha ugumu wa kazi zao.
Mwandishi: Sudi Mnette RNA/RFI/RSF
Mhariri: Iddi Ssessanga