1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwendesha mashtaka: Pistorius apewe miaka kumi jela

17 Oktoba 2014

Upande wa mashtaka katika kesi ya Oscar Pistorius unataka mwanariadha huyo mashuhuri wa Afrika Kusini anastahili kufungwa jela kwa angalau miaka 10 baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mchumba wake Reeva Steenkamp

https://p.dw.com/p/1DXwY
Oscar Pistorius Gericht Pretoria
Picha: Reuters/M. Hutchings

Mwendesha mashtaka Gerrie Nel ameiambia mahakama katika kikao cha kusikiliza hukumu ya Pistorius, kuwa adhabu ya chini jamii inaweza kuridhika nayo ni kipindi cha miaka kumi jela.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, yaani upande wa mashtaka na wa mshtakiwa, jaji Thokozile Masipa anatarajiwa kutangaza hukumu Jumanne wiki ijayo.

Wakili wa mshtakiwa Barry Roux alisema kuwa Pistorius, “hakufanya mauaji ya makusudi bila kuwa na hisia zozote” na anastahili kupewa kifungo cha nyumbani badala ya kupelekwa jela. Lakini Nel alitaja pendekezo hilo kuwa la “kutisha mno na lisilowiana na uzito wa kesi”. Alisema "Hoja yangu ni kuwa suala hili ni nzito, na jamii inataraji kifungo cha jela na mshtakiwa apewe kifungo cha jela. Nimekuwa mahakamani kwa muda mrefu kuweza kupendekeza 20 nikitumai mahakama itafikia 10, lakini sifanyi hilo. Kifungo cha chini ambacho jamii itafurahia ni miaka 10 jela".

Pistorius mwenye umri wa miaka 27 aliondolewa mashtaka ya kumuua Steenkamp kwa kufyatua risasi tatu kupitia mlango wa choo nyumbani kwake mjini PRETORIA mwaka jana, lakini akapatikana na hatia ya kuua bila kukusudia, kosa ambalo adhabu yake inaweza kuwa ni kutozwa faini, au kupewa kifungo cha hadi miaka 15 jela.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu