1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenge wa Olimpiki waanza safari Moscow

7 Oktoba 2013

Safari ya mwenge wa michezo ya Olimpiki ya majira ya barafu mjini Sochi, imeanza rasmi Moscow, na itapitia katika miji mingi ambayo itaonyesha utajiri wa kihistoria, utamaduni na makabila ya Urusi

https://p.dw.com/p/19vm5
Wanariadha wa Urusi wakiwa na mwenge wa Olimpiki mbele ya Ikulu ya Rais mjini Moscow, Kremlin
Wanariadha wa Urusi wakiwa na mwenge wa Olimpiki mbele ya Ikulu ya Rais mjini Moscow, KremlinPicha: Kirill Kudryavtsev/AFP/Getty Images

Kumekuwepo na hisia tofauti kuhusiana na michezo ya Olimpiki ya majira ya barafu itakayoandaliwa mjini Sochi nchini Urusi hapo mwakani, na hasa kuhusiana na madai ya serikali ya Urusi kuwakamata mamia ya wafanyakazi ambao ni wahamiaji nchini humo, na pia kuwafukuza wengine wao kwa madai ya kukiuka sheria za uhamiaji au ajira.

Rais wa Urusi Vladmir Putin wakati akiuwasha mwenge huo hapo jana, amesema safari hiyo ya miezi minne ya mwenge wa Olimpiki “itauonyesha ulimwengu jinsi Urusi ilivyo na jinsi wanavyoipenda”. "Ni kweli kwamba Warusi wanapenda michezo sana na wanafurahia chochote kinachohusiana nayo. Bila kuwepo uungaji mkono kutoka kwa umma, raia wa URUSI, ingekuwa vigumu kutekeleza miradi mikubwa ya michezo. Michezo ya Olimpiki ya Sochi imekuwa ndoto yetu ya pamoja ambayo sasa inatimia".

Na jambo la kushangaza hata zaidi ni kwamba Maafisa wa Urusi pia walitaka kuusafirisha mwenge huo katika anga za juu… mpango huo hata hivyo ulifutwa kwa sababu za kiusalama, lakini, mwenge wa Olimpiki ambao hautawashwa, utapelekwa moja kwa moja hadi katika Kituo cha Kimataifa cha Anga za Juu mnamo Novemba 7, ambako wanaanga wawili wa Urusi watautembeza angani kabla ya kurejeshwa duniani mnamo Novemba 11. hmmm bila shaka hilo ni tukio la kipekee…

Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman