Mwisho wa kuwasilisha majina ya wagombea Kenya
21 Januari 2013Saa 11:00 leo jioni ndio saa ya mwisho kwa vyama vya kisiasa kuwasilisha orodha ya wagombea kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) huku vyama vikuu TNA na ODM vikifanya kila viwezalo kusuluhisha mizozo iliyotokea wakati wa kura ya mchujo mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi wa bodi ya kitaifa ya uchaguzi katika chama cha ODM Franklini Bett amesema kwamba chama chake kitarekebisha kila mapungufu yaliyojitokeza “Ningependa kushughulikia malalamiko kuhusu Dk. Oburu na mpinzani wake na kati ya Jakoyo Midiwo na mpinzani. Nilitaka kushughulikia hayo na mengine ambayo yanahitaji kushughulikiwa kwa dharura”. Alisema
Wagombea wengi walalalamika
Wagombea wengi hawakuridhishwa na matokeo ya uteuzi huo na hivyo kusababisha ghasia na vurugu. Mkoa wa Nyanza ambao ni ngome kuu ya chama cha ODM ndio ulioathiriwa zaidi.
Ghasia zilizuka huko Siaya baada ya Oburu Odinga, kaka yake Waziri Mkuu Raila Odinga, kutangazwa mshindi kuwania kiti cha ugavana, na dada yake kutangazwa mshindi kuwania kiti cha ugavana jimbo la Kisumu kwa tikiti ya chama cha ODM.
Kwingineko huko Mkoa wa Kati ngome kuu ya chama cha TNA kinachoongozwa na Uhuru Kenyatta mambo hayakuwa tofauti. Nako pia walioshindwa hawakuweza kukubali matokeo. Watu wengi sasa wanasema vyama vya kiasasa havina uwezo wa kuendesha uchaguzi wa kitaifa wa huru na haki bila usaidizi kutoka kwa taasisi zilizo na uzoefu wa kuendesha shughuli kama hiyo.
Hivyo basi wengi wanahoji kwamba shughuli hiyo ingeachiwa tume ya uchaguzi nchini lakini kuamabata na sheria tume ya uchaguzi jukumu lake ni kuendesha uchaguzi mkuu pekee.
Shaka ya uchaguzi wa Machi 4
Kivumbi kinatarajiwa wakati wa uchaguzi mkuu hapo Machi 4 wenyewe kwani wengi wa wagombea walioshindwa wamerudi tena uwanjani kutumia tikiti ya vyama vingine hata ingawa vyama wanavyosimama navyo si maarufu.
Idara ya polisi imetumia kura hii ya mchujo kama kigezo cha kujiandaa vilivyo kukabiliala na visa vya ghasia wakati wa uchaguzi mkuu ujao. Tume ya uchaguzi IEBC imesema wazi kwamba itachukua tu majina ya wagombea waliokuwa wameteuliwa na vyama kufikia saa sita usiku wa Ijumaa tarahe 19 kwa mujibu wa sheria.
Swali ni je waliohamia vyama vya kisiasa baada ya tarehe 19 wataenda wapi? Jawabu linasubiriwa saa kumi na moja leo jioni wakati IEBC itakapopokea orodha za wagombe kutoka kwa vyama vya kisiasa.
Mwandishi: Alfred Kiti
Mtayarishaji: Grace Patricia Kabogo
Mhariri: Mohammed Khelef