1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yajipanga kuwashughulikia wakimbizi

10 Novemba 2015

Mawaziri wa mambo ya ndani wa nchi za Umoja wa Ulaya wameahidi kuchukua hatua za haraka kushughulikia mzozo wa wakimbizi, na kuepusha janga la kibinadamu kwa wahamiaji linaloweza kusababishwa na msimu wa baridi kali.

https://p.dw.com/p/1H2dZ
Ulaya inakabiliwa na wimbi la wakimbizi, kubwa zaidi tangu kumalizika kwa vita vya pili
Ulaya inakabiliwa na wimbi la wakimbizi, kubwa zaidi tangu kumalizika kwa vita vya piliPicha: Reuters/S. Zivulovic

Mkutano wa mawaziri hao usio wa kawaida umefanyika siku mbili tu kabla ya mwingine utakaokutanisha Ulaya na Afrika kisiwani Malta, ambao utatafakari njia za kupunguza idadi ya wahamiaji wanaoingia barani Ulaya kupitia Libya. Njia hiyo ni ya pili kwa kupitisha wahamiaji wengi, baada ya ile inayoanzia Uturuki kupitia Ugiriki na mataifa ya Ukanda wa Balkan.

Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imekuwa ikiziwekea shinikizo nchi wanachama, ikizishutumu kwa kujivuta katika kudhibiti mipaka yao ya nje, na kujenga vituo vya kushughulikia maombi ya hifadhi kutoka kwa wakimbizi wanaoingia Ulaya. Nchi hizo pia zimekosolewa namna zinavyoendesha mchakato wa kuzipunguzia mzigo wa wahamiaji nchi za mpakani kama vile Italia na Ugiriki.

Kitisho cha majira ya baridi

Wakati majira ya baridi kali yakibisha hodi barani Ulaya, waziri wa mambo ya ndani wa Luxembourg, nchi ambaye kwa sasa inashikilia urais wa kupokeza wa Umoja wa Ulaya amesema inabidi kila juhudi zifanyike kuepusha balaa la kibinadamu.

Mawaziri wa mambo ya ndani wa EU wakikuna vichwa kutokana na mzozo wa wakimbizi
Mawaziri wa mambo ya ndani wa EU wakikuna vichwa kutokana na mzozo wa wakimbiziPicha: picture-alliance/AP Photo/G. Wijngaert

Waziri huyo Jean Asselborn amesema Ulaya itajitahidi kuepusha vifo vya wahamiaji baharini, na haitaruhusu watu hao kufa kwa baridi katika nchi za Balkan.

Idadi ya wahamiaji wanaoingia Ulaya iliongezeka sana mnamo majira ya joto, wengi wa wale wanaoingia wakiwa wanakimbia vita na umasikini katika nchi za Mashariki ya Kati kama vile Syria, Irak na Afghanistan.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere amesisitiza msimamo kuwa watu wanaotoka Afghanistan hawatopewa hifadhi ya ukimbizi.

''Wasiwasi mkubwa kwa Ujerumani, na kwa Ulaya ni idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Afhganistan. Hatutaki wasambazwe, lakini tunawapa ujumbe ufuatao: Baki nchini mwenu, kwa sababu Ulaya imejipanga kuwarudisha huko moja kwa moja kutoka Italia na Ugiriki''. Amesema waziri de Maiziere.

Ulaya kutafuta muafaka na Afrika

Kamisheni ya Ulaya ilipendekeza mpango wa kudumu kuhusu mzozo wa wakimbizi baada ya wakimbizi takriban 800 kuzama baharini wakiwa njiani kutoka Libya kuelekea Italia mwezi Mei mwaka huu.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Thomas de MaizierePicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Katika wimbi hili la wakimbizi ambalo ni kubwa zaidi tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia, wahamiaji karibu 800,000 wamefanikiwa kuingia barani Ulaya, na wengine wapatao 3000 wamezama katika bahari ya Mediterania wakiwa njiani kuelekea huko.

Wingi wa wakimbizi hao umepunguza uungwaji mkono wa kuwapokea katika nchi kama Ujerumani na Sweden ambazo awali zilionyesha utashi mkubwa.

Katika mkutano wa kesho Jumatano nchini Malta, ambao utahudhuriwa na viongozi wapatao 50 kutoka Ulaya na Afrika, viongozi wa Ulaya watazitaka nchi za Afrika kuwapokea watu wao waliokwenda Ulaya kwa sababu za kiuchumi.

Ulaya inatarajiwa kuahidi euro bilioni 3.6 kwa Afrika zitakazotumiwa katika kupambana na umasikini na kusuluhisha mizozo, sababu mbili ambazo zinaongoza kuwafanya waafrika wazihame nchi zao na kukimbilia Ulaya.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri:Josephat Charo