Mzozo wasababisha malori kukwama mpaka wa Rwanda na DRC
31 Januari 2020Malori takribani 200 yanayosafirisha bidhaa kutoka nchi za Afrika mashariki kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yamekwama kwenye mpaka kati ya Rwanda na Congo kwa wiki nzima sasa, baada ya vijana kuchimba shimo kubwa katikati mwa barabara hiyo inayounganisha mataifa hayo kuishinikiza serikali iifanyie ukarabati barabara hiyo.
Kwa muda wa wiki moja sasa, vijana wanaamka kila mapema asubuhi na kuelekea Giamba kwenye barabara inayotoka kwenye mpaka wa Ruzizi ya pili kuelekea eneo linaloitwa "Essence Major-Vangu", ili kuwasilisha malalamiko yao kwa viongozi. Wanasema hawaelewi kwa nini kazi za kukarabati barabara yenye urefu wa kilomita mbili na nusu imeshindikana, ijapokuwa kazi za ukarabati ilitangazwa tangu myaka kadhaa.
Kufungwa kwa barabara hiyo kunawaathiri madereva wa malori yanayotoka hasa nchi za Ethiopia, Uganda, Kenya, Tanzania na Zambia kuja hapa Bukavu. Wameelezea kuwa katika hali mbaya wanaposubiri hasira za vijana hao zituliye, na wameiomba pia serikali ikarabati barabara hiyo muhimu kwa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Gavana wa mkoa wa kivu kusini Théo Ngwabidje Kasi alikutana na vijana waandamanaji na kuwataka kuwa wavumilivu. Ameahidi kwamba kazi ya kukarabati wa barabara hii itaanza Jumamosi hii.
Ikiwa kazi ya kutengeneza barabara ya Giamba haitafanyika na kumalizika inavyo stahili, vijana wa Bukavu wameahidi kufanya maandamano ya zaidi.