Mzozo watokota Burundi kuelekea uchaguzi mkuu
17 Februari 2014Tukio hilo linaonekana kusababisha pia kupamba moto zaidi kwa mzozo wa kisiasa ambao umekuwa ukitokota nchini humo wiki za hivi karibuni, wakati Burundi ikielekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani.
Polisi waliyazingira makao makuu ya chama cha UPRONA ambacho ni mshirika katika serikali chini ya makubaliano ya kugawana madaraka yaliyofikiwa ili kumaliza uhasama wa kikabila yaliyokomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2005.
Wanachama wa UPRONA waliokuwa wakiwasilia kwa mkutano wa kuwachagua viongozi wapya wa chama hicho walizuiwa kuingia katika makao makuu ya chama chama na watatu kati yao walijeruhiwa walipojaribu kukaidi maagizo ya askari.
Mkutano wa UPRONA wasambaratishwa
Waziri wa mambo ya ndani wa Burundi Edouard Nduwimana amesema polisi walizuiwa mkutano huo kufanyika kwasababu ulikuwa kinyume na sheria.Hata hivyo wanachama wa UPRONA wamewashutumu maafisa wa serikali kwa kujaribu kuzua migawanyiko ndani ya chama hicho na kuzuwia kuchaguliwa kwa viongozi wapya ambao wametofautiana na Rais Pierre Nkurunzinza na chama chake CNDD FDD.
Mzozo uliibuka baada ya Rais Nkurunzinza kupendekeza kuifanyia marekebisho katiba ili kumruhusu kugombea kwa mara ya tatu urais na kubadilisha makubaliano ya kugawana madaraka.Wapinzani wake kikiwemo chama cha UPRONA kimesema hatua hizo zitawatenga walio wachache nchini humo kutoka jamii ya watutsi.
Mzozo watishia udhabiti
Mawaziri watatu wanaotokea chama cha UPRONA walijiuzulu mapema mwezi huu baada ya Rais kumfuta kazi makamu wake wa rais ambaye ni mtutsi na mwanachama wa UPRONA.Hali hiyo ya taharuki iliongezeka hata zaidi Ijumma iliyopita baada ya Nkurunzinza kumteua Prosper Bazombanza kuwa makamu wake licha ya kupingwa na chama chake UPRONA kuchukua wadhifa huo.
Wakereketwa wanasema Bazombanza ameteuliwa kwasababu anaunga mkono juhudi za Nkurunzinza za kuifanyia mageuzi katiba ili kugombea urais.Wanachama wa UPRONA wamesema hawautambui uteuzi huo kwani hakuidhinishwa na chama. Uchaguzi wa rais na bunge nchini humo unatarajiwa kufanyika 2015.
Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Afp
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman