1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nüremberg na Bayern Munich zaumana leo

Ramadhan Ali25 Agosti 2006

Kombe la klabu bingwa barani Afrika limerudi uwanjani mwishoni mwa wiki hii na kura imepigwa ya champions League-kombe la klabu bingwa barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/CHdJ

Bundesliga-ligi ya Ujerumani, inarudi uwanjani mwishoni mwa wiki hii,huku mashabiki wakiukodolea macho mpambano wa jumamosi wa kukata na shoka kati ya timu mbili za Bavaria-mabingwa Bayern Munich, na viongozi wa Ligi FC Nuremberg.Nüremberg ndio inayoongoza Ligi ya ujerumani tangu kuanza msimu wiki tatu zilizopita:

Jioni hii basi, Nuremberg inaitembelea mabingwa Bayern Munich katika Alllianz Arena na mshindi ataparamia kileleni mwa ngazi ya Ligi.Makamo bingwa Werder Bremen walikuwa uwanjani jana walipopambana na Schalke katika changamoto nyengine ya kusisimua mwishoni mwa wiki hii.

Bayer Leverkusen inacheza nyumbani na Wolfsburg wakati B.Moenchengladbach ina miadi na Armenia Bielefeld.Hannover 96 inakumbana na Alemania Aaachen iliopanda daraja ya kwanza msimu huu wakati Stuttgart ina kazi ngumu nyumbani ikipapurana na Borussia Dortmund.Bochum inatimuana wakati huu na Cottbus.Kesho itakua zamu ya Mainz kuchuana na Energie Cottbus wakati Hertha Berlin, itaitembelea Hamburg.

Hambgurg kati ya wiki hii ilikata tiketi ya tatu kwa klabu za ujerumani kushiriki katika champions League-kombe la klabu bingwa barani ulaya.Kufuatia duru hiyo, kura ikapigwa juzi kuamua makundi mbali mbali:Mabingwa FC Barcelona ya Spain imeangukia kundi moja na mabingwa wa Uingereza Chelsea,makamo-bingwa wa Ujerumani Werder Bremen na Lowski Sofia ya Bulgaria.

Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich wanakutana na Inter Milan ya Itali, Sporting Lisbon ya ureno –mabingwa wa 2004 na Spartak Moscow.

Mabingwa wa mwaka 2005 Fc Liverpool ya uingereza wana miadi na PSV Eindhoven ya holland,Girondons Bordeaux ya Ufaransa na Galatasary Istanbul ya Uturuki.

Real Madrid ya Spian, imo kundi moja na Olympic Lyon ,Steau Bukarest na Dynamo Kiev.

Manchester United ya Uingereza iko kundi moja na Celtic Glasgow ya Scotland,Benefica Lisbon na FC Copenhagen za Ubelgiji na Denmark zakamilisha kundi hilo.

Arsenal London na FC porto,ZSKA Moscow wanajumuika na Hamburg katika kundi G.Ac Milan ,Lille ya Ufaransa na AEK Athen na RSC Anderlecht zakamilisha makundi yote.

Ufaransa imefaulu kuwabakisha Liliam thuram na Claude Makelele kuendelea kuichezea timu ya taifa.Nahodha lakini anabakia kuwa Patrick Vieira aliechukua usukani kutoka kwa Zinedine Zedane aliestaafu kabisa .Viera alikwishachaguliwa nahodha pale Zidane alipostaafu mara ya kwanza 2004 kabla kurejea tena kuichezea Ufaransa.

Wengine walidhania Lilian Thuram, angefaa kushika unahodha.Lakini Thuram alikwisha mara mbili kuiongoza Ufaransa na sasa ana umri wa miaka 34,beki huyu mshahara iliosalia ni kufuata nyayo za Zidane na kustaafu.Lakini,kocha Domenech anamhitajia kama vile Makelele kuiokoa Ufaransa katika zahama ya kuania tiketi za kombe lijalo la Ulaya 2008.

Tukigeukie dimba barani Afrika:Simba wa nyika-Kameroun, wameamua kupiga kambi yao ya mwisho nchini Kenya kabla kuwasili Kigali, mwishoni mwa wiki ijayo kwa changamoto na Ruanda katika kinyan’ganyiro cha kuania tikiti za finali ya Kombe la afrika la mataifa 2008 nchini Ghana.

Kikosi cha wachezaji 18 kikujumuisha staid wa FC Barcelona, Samuel eto’0 na wachezaji wengi wanaocheza n’gambo ,chatazamiwa kuwasili Nairobi jumaane kwa kambi ya siku 4.

Simba wa nyika wataondoka Nairobi ijumaa, tarehe mosi Septemba, kuelekea Kigali.Wiki iliopita tu, Arie Haan kutoka Holland, aliecheza kombe la dunia, 1974 katika kikosi cha nahodha Johan Cryff, aliteuliwa kuwa kocha mpya wa samba wa nyika baada ya kujiuzulu kwa mreno Artur Jorge hapo machi mwaka huu pale Kamerun ilipopigwa kumbo nje ya nusu-finali ya Kombe la Afrika la mataifa nchini Misri.Simba wanyika walishindwa pia kunyakua tiketi ya Kombe la dunia nchini Ujerumani.

Nae Quinton Fortune, anaeichezea sasa Bolton Wanderers ya Uingereza, anarejea kuichezea Bafana Bafana kwa mara ya kwanza tangu Machi mwaka jana .

Fortune ameteuliwa katika kikosi cha wachezaji 19 kwa changamoto ya mwishoni mwa wiki ijayo ya kombe la Afrika kupambana na Congo.Anaerejea pia katika kikosi cha Bafana Bafana ni Beni Mccathy.

Bafana bafana wana miadi na Congo-Brazzaville, mjini Johannesburg ,lakini hawatasimamiwa na kocha mpya Alberto Parreira wa Brazil,bali na kocha wa mpito Pitso Mosimane.Parreira anaeanza kazi mapema mwakani, hatahivyo, atakuwa uwanjani mjini Johannesberg kuangalia mechi hiyo ya jumamosi ijayo.

Leo na kesho, kinyan’ganyiro cha kombe la klabu bingwa barani Afrika kinaendelea:

Al Ahli ya Misri ina miadi leo na Asante Kotoko ya Ghana wakati CS Sfaxien ya Tunisia inawakaribisha leo nyumbani JS Kabylie ya Algeria katika changamoto za kundi A.

Ama katika kundi B, kesho, Enyimba ya Nigeria inakumbana na ASEWMC mimosas iliodai mlinzi wake mashuhuri Abubakar Baleria, ametoweka muda mfupi kabla changamoto ya kesho.Hearst of Oak ya Ghana inakutana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Rais wa Enyimba, Anyansi Agwu,aliarifu kwamba Baleria hakupewa ruhusa ya kuondoka na wanadhani ametoroshwa na dalali anaeuza wachezaji.Kesho,Enyimba itabidi kupania bila ya mlinzi wake kufuta madhambi ya mabao 3:0 waliofanya Abidjan, walipokutana na Asec mara iliopita.