Nairobi. Somalia, Ethiopia na Eritrea bado zatupiana lawama.
14 Aprili 2007Maafisa wa Somalia, Ethiopia na Eritrea wamekuwa wakishutumiana jana Ijumaa kuhusiana na majukumu yao katika mzozo wa Somalia, na kuonyesha wasi wasi kuwa Somalia inaweza kuhatarisha eneo la pembe ya Afrika.
Tofauti hizi zimeelezwa zaidi katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa mkutano wa kimkoa uliofanyika mjini Nairobi.
Mawaziri wa nchi hizo wamesema kuwa wana wasi wasi juu ya kuongezeka kwa ghasia katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, kutokana na kuendelea kuongezeka kwa matukio ya ghasia yanayofanywa na makundi yenye msimamo mkali na kusababisha upotevu mkubwa wa maisha ya watu na watu kukimbia makaazi yao.
Shirika la umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR limesema jana kuwa idadi ya watu ambao wanaukimbia mji wa Mogadishu imeongezeka na kufikia 208,000 kutoka 124,000 wiki moja iliyopita.