Wanamibia wanamchagua rais wao katika uchaguzi wa leo
27 Novemba 2024Hiyo ni wakati chama chake cha SWAPO kikikabiliwa na ushindani mkali unaotishia udhibiti wake wa miaka 34 madarakani. Nandi-Ndaitwah mwenye umri wa miaka 72, wa chama cha South West Africa People's Organization alipiga kura yake katika mji mkuu Windhoek na kuwatolea wito wapiga kura milioni 1.5 waliosajiliwa wajitokeze kwa wingi vituoni. Chama cha SWAPO kimeitawala nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini tangu uhuru mwaka 1990 lakini, huku kukiwa na malalamiko kuhusu ukosefu mkubwa wa ajira na ukosefu wa usawa, Nandi-Ndaitwah anaweza kulazimishwa kuingia katika duru ya pili ya uchaguzi kama atashindwa kupata angalau nusu ya kura. Ana wapinzani wanne wakuu akiwemo Panduleni Itula, mwenye umri wa miaka 67, ambaye ni daktari wa zamani wa meno na mwanasheria aliyeanzisha chama cha Independent Patriots for Change mwaka wa 2020. Itula alipata asilimia 29 ya kura katika uchaguzi wa 2019, aliposhindwa na kiongozi wa SWAPOHage Geingob, aliyepata asilimia 56 ya kura.