1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani aling'ara na nani alishindwa kutamba AFCON?

12 Februari 2013

The Super Eagles ndio mabingwa wapya wa soka barani Afrika baada ya kunyakua kombe la Mataifa Bingwa Afrika AFCON nchini Afrika Kusini. Lakini jee, ni kina nani waliong'ara na walioshindwa kutamba katika dimba hilo?

https://p.dw.com/p/17c3a
Nigeria's players celebrate winning their African Nations Cup (AFCON 2013) final soccer match against Burkina Faso in Johannesburg February 10, 2013. REUTERS/Siphiwe Sibeko (SOUTH AFRICA - Tags: SPORT SOCCER)
Fußball Nationalmannschaft NigeriaPicha: Reuters

Kwanza waliotamba ni Burkina Faso ambao walifuzu katika fainali, katika mazingira ambayo hayakuonekana kuwa rahisi, ikizingatiwa kwamba 16 kati ya kikosi chake cha wachezaji 23 walishiriki dimba la mwaka wa 2012, na wakabanduliwa nje katika duru ya kwanza baada ya kushindwamara tatu mfululizo. Lakini tunamvulia kofia mkufuzi Mbelgiji Paul Put kwa kukipiga msasa kikosi chake.

Pia hongera kwa shirikisho la soka Afrika CAF kwa kushughuli haraka kuhakikisha kwamba haki inatendeka kwa mwathiriwa wa tukio la kadi nyekundu mshambuliaji wa Burkina Faso Jonathan Pitroipa ambaye aliruhusiwa kucheza fainali.

Kikosi cha Cape Verde kiliwashangaza wengi
Kikosi cha Cape Verde kiliwashangaza wengiPicha: picture-alliance/empics

Cape Verde tunawapa kongole kwa kuwakaba mabingwa wa zamani Afrika Kusini na Morocco, baada ya kupata ushindi dhidi ya Angola na wangewashinda Ghana katika robo fainali kama wangekuwa na bahati nzuri na kutumia nafasi zao vyema. Miongoni mwa waliofanya vibaya ni Cote d'Ivoire ambayo ina kikosi cha wachezaji nyota wengi kama vile nahodha Didier Drogba, makaka Kolo na Yaya Toure, na Didier Zokora. Watakwenda katika madaftari ya kumbukumbu kama timu iliyoshindwa kutamba katika AFCON na watajilaumu wenyewe. Ghana pia walipigiwa upatu kushinda kombe hilo lakini wakashindwa na wapinzani walioonekana kuwa hafifu. Eneo la Uarabuni pia linafahamika kufanya vyema lakini Morcco, Tunisia na Algeria zilizembea na ilhali zinajulikana kuwa moto wa kuotea mbali. Kisha tunafahamu kuwa ilikuwa vigumu kutaraji mabingwa watetezi Zambia kusalia na taji, lakini Chipolopolo wa Zambia walitoka mapema mno katika dimba hilo.

Champions League

Kwingineko Manchester United itarejelea utani wake wa tangu jadi na Real Madrid Jumatano wiki hii huku mkufunzi Jose Mourihno akiutaja mchuano huo unaosubiriwa kwa hamu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kuwa ni mpambano ambao “ulimwengu mzima unausubiri”.

Celtic na Barcelona wanakabiliwa na mtihani mgumu
Celtic na Barcelona wanakabiliwa na mtihani mgumuPicha: picture-alliance/dpa

United, mabingwa mara tatu wa Champions League wanakwenda nyumbani kwa Madrid, ambao wanashikilia rekodi ya kuwa na kombe hilo mara tisa. Katika mchuano wao wa mwisho kati ya watani hao wawili, Real waliwanyuka United jumla ya magoli sita kwa matano katika mechi ya kukata na shoka ya mikondo miwili, ya robo fainali mnamo mwaka wa 2003. Mourinho anasema ulimwengu hausubiri mechi nyingine zozote ila mchuano baina yao na watafanya kila wawezalo kuwapa watazamji kile wanachotaka.

Nao mabingwa wa Scotland Celtic ambao wamekuwa timu ya kwanza ya Uingereza kushinda kombe hilo mwaka wa 1967, waliwaduwaza wengi kwa kufika 16 za mwisho na wana matumaini halisi ya kuonyesha mchuano mzuri dhidi ya mabingwa mara tatu Juventus. Paris Saint Germain wanakwenda nyumbani kwa Valencia ambao walifika fainali mnamo mwaka wa 200 na 2001 katika mchuano mwingine wa Jumanne. Jumatano, Borussia Dortmund, ambao walishinda katika kundi lao mbele ya Real Madrid, wanatarajia kusajili matokeo mazuri kama ushindi wao wa mwaka 1997. Mkufunzi Jurgen Klopp atalazimika kufanya marekebisho kikosi chake ambacho kinayumba nyumbani, wakati watakaposafiri kuchuana dhidi ya Shakhtar Donetsk ambao waliwabandua mabingwa watetezi Chelsea katika awamu ya makundi.

Mechi hizi nane zinakamilisha wiki ya kwanza ya uhondo ambapo timu zilizomaliza katika nafasi za pili katika makundi yao zinacheza mkondo wa kwanza nyumbani kabla ya mechi za marudiano kuanza Machi tano na sita. Mashabiki wa Barcelona watalazimika kusubiri hado Februari 20 kabla ya kupambana na AC Milan uwanjani San Siro. Bayern Munich ambao wanawaangamiza wapinzani wao katika Bundesliga watakabiliwa na kibarua kigumu uwanjani Emirates kupambana na Arsenal. Kwingineko Porto watakabana koo na Malaga. Galatasaray watapeperusha bendera ya Uturuki katika juhudi za kuleta nyumbani kombe hilo la Ulaya kwa mara ya kwanza, na kuwasili Didier Drogba na Wesley Sneijder kumeongeza matumaini katika klabu hiyo ya Istanbul. Schalke 04 ya Ujerumani ndio watakaoangushana na miamba hao wa Uturuki.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/Reuters/DPA

Mhariri: Mohammed Khelef