Nani anapambana na nani katika Champions League
12 Desemba 2014Wakati zikiwapo timu tisa ambazo zimewahi kutwaa taji la Champions League katika miaka 11 iliyopita , hakuna anayeweza kuishutumu Champions League kwa kuweza kutabirika.
Inaonekana hata hivyo, kwamba kundi la vigogo vinne , Big 4, limeundwa katika mashindano haya ya vilabu barani Ulaya, na awamu ya makundi msimu huu inaunga mkono nadharia hiyo.
Barcelona, Chelsea, Bayern Munich na mabingwa watetezi Real Madrid , mabingwa wanne wa mwisho wa tuzo hilo kubwa la soka la Ulaya kwa vilabu , wamekuwa wa kwanza katika makundi yao, katika michezo iliyomalizika siku ya Jumatano.
Vigogo vinavyotamba Ulaya
Katika misimu mitatu iliyopita , takriban vigogo vitatu katika hivyo vinne vimefanikiwa kufikia nusu fainali ya Championsd League. Madrid na Barcelona zimefanya hivyo katika mwaka 2011.
Kwa hiyo wakati tukielekea katika awamu ya mtoano ambayo itaanza Februari mwakani , itakuwa mshangao mkubwa iwapo mabingwa wa msimu huu hawatafika katika kundi hili dogo la vigogo wanne, timu ambazo kwa sasa zinaonesha viwango ambavyo ni tofauti na timu nyingine zilizobaki.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman