1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani ataongoza dunia iwapo Trump ataitoa Marekani?

24 Januari 2017

Mkakati wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kufuata sera ya "Marekani kwanza" unaanza kuzusha maswali juu ya nani atajaza ombwe iwapo Marekani itajivua jukumu la uongozi wa dunia.

https://p.dw.com/p/2WKGr
USA steigen aus Transpazifik-Handelsabkommen aus
Picha: Reuters/K. Lamarque

China na Urusi ni miongoni mwa nchi zinazowania kuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika masuala ya uchumi na kijeshi, huku Ujerumani inaweza kujitokeza kama kiongozi wa kimaadili wa mataifa ya Magahribi.

Kwa vizazi kadhaa Marekani imekuwa ikitoa miongozo ya uchumi wa dunia, kufuatilia na kushughulikia vitisho vya kiusalama kimataifa, na kuogoza miitikio ya dunia kwa migogoro kama mripuko wa Ebola na tetemeko la ardhi nchini Haiti.

Lakini baada ya kuingia madarakani kwa ujumbe unaoashiria kujitenga wenye msingi wake katika dhana kwaba Marekani inahitaji kushughulikia mambo yake yenyewe, Trump amesema na kufanya kidogo kuondoa fikira kwamba anataka mataifa mengine yashughulikie matatizo yao wenyewe.

Katika hotuba yake ya kuapishwa, Trump alisema Marekani kwa muda mrefu imewekeza katika viwanda, majeshi, mipaka na miundimbinu ya mataifa mengine, huku vya kwake vikiachwa kuzorota. "Hayo yamepita," alisema Trump.

Abatilisha mkataba wa TTP

Katika mmoja ya hatua zake za kwanza kabisaa, Trump aliiondoa rasmi Marekani katika makubaliano ya biashara ya mataifa ya kanda ya Pacific TPP, mradi ulioanzishwa chini ya utawala wa Rais Goerge Bush na kujadiliwa na Rais Barack Obama ili kuweka sheria za biashara kati ya Marekani na mataifa ya Asia na kukabiliana na ushawishi wa kiuchumi wa China.

Trump alisema alikuwa akiwafanyia jambo zuri wafanyakazi wa Marekani kwa kuuvunja mkataba wa TPP. Lakini Mrepublican mwenzake Seneta John McCain alisema kujiondoa katika mkataba huo ni kukabidhi uongozi wa Marekani barani Asia kwa China. Na China siyo nchi pekee inayoweza kunufaika na kubana matumizi kwa Marekani.

USA Präsident Trump frühstückt mit Wirtschafts-Bossen
Donald Trump alipokutana na wafanyabiashara wakubwa wa Marekani kuwataka wahamishie uzalishaji nchini Marekani. Ni katika kutimiza ahadi yake ya Marekani kwanza.Picha: picture alliance/AP Photo/P. Martinez Monsivais

Kwa njia zao wenyewe Urusi na Ujerumani zinaweza kutumia fursa hiyo kuongeza ushawishi wao duniani. Lakini hakuna anayeweza kufikia kwa wakati mmoja nguvu ya Marekani kiuchumi, kijeshi, na kimaadili, na Marekani inapojitenga zaidi hii inamaanisha ombwe la uongozi.

"Hakuna taifa au kundi la mataifa linaloweza kufanya kile ambacho Marekani imekifanya katika kipindi cha nusu karne iliopita," alisema Jon Alterman, afisa wa zamani wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, ambaye kwa sasa yuko katika kituo cha utafiti wa masuala ya kimataifa na kimkakati. Alisema hili ni suala la rasilimali kwa sehemu moja, na la kimalengo kwa sehemu nyingine.

Ujerumani yahofia kuangalia kama mfano

Wakati washindani wa Marekani - Urusi na China zingefurahia fursa yoyote ya kujaribu kuchukuwa nafasi ya Marekani, nchi nyingine barani Asia, Ulaya na kwingineko wanasumbuliwa na uwezekano wa Marekani kujivua uongozi wake. Hata Ujerumani ina wasiwasi kuhusu kuangaliwa zaidi kama mfano wa kimaadili.

China ambayo imewekeza mabilioni barani Afrika na Amerika Kusini ili kuwa na ushawishi katika ulimwengu unaoendelea, inaweza kugeuka taifa lenye ushawishi mkubw wa kiuchumi. Tayari China iko katika mchakato wa kufukia makubaliano makubwa ya kibiashara na mataifa kadhaa ambayo huenda yakawa makubaliano mbadala kwa TPP, jambo ambalo utawala wa Obama ulionya litaiacha China kutunga sheria na kuharibu kabisaa viwango vya ajira na mazingira.

Beijing ilitumia kutawazwa kwa Trump kama fursa kudhihaki demokrasia ya Marekani na kupigia debe mfumo wake wa kikomunisti kuwa ndiyo bora. Na wengi wa majirani za China wanashiriki hofu yake kuhusu vitisho vya Trump kuanzisha vita vya kibiashara na taifa hilo kubwa kabisaa la Asia kwa kuzitoza kodi kubwa bidhaa za kutoka China.

Hata ushirika wa kijeshi wa Marekani siyo jambo la uhakika pia. Trump amependekeza kuwepo mtazamo mpya mpana, akiitaja jumuiya ya kujihami NATO kuwa iliopitwa na wakati na kuwapa changamoto washirika wa Marekani kugharimia zaidi ulinzi wao, wakati ambapo Urusi ikizidi kujiimarisha Ulaya Mashariki, ambayo iliteseka sana wakati wa utawala wa Kisoviet.

China Donald Trump auf Titelseite einer Zeitschrift
Jarida lenye picha ya Trump katika duka mjini Beijing, China. China inatazamiwa kunufaika kutoka na mkakati wa Trump kuiondoa Marekani kwenye uongozi wake wa dunia.Picha: Getty Images/AFP/G. Baker

Utandawazi dhidi ya utengano

Msukumo wa Trump umeakisi mjadala mpana wa dunia kuhusu utandawazi dhidi ya utengano. Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May atamtembelea Trump baadae wiki hii, akitaka ushirikiano kutoka kwa kiongozi wa Marekani alieshangilia kura ya nchi yake kujitoa katika Umoja wa Ulaya, ambayo Obama alipiga kampeni kuipinga.

Wakati nguvu zinazoongezeka za kiuchumi za China na nguvu za kijeshi za Urusi vinawezakuwavutia baadhi, mataifa machache yanayoegemea upande wa Magharibi yatakwenda kwa mataifa hayo kupata uongozi wa kimaadili. Ujeurmani imajaribu kujaza ombwe hilo, ikiwapokea mamia kwa maelfu ya wakimbizi na kuongoza harakati za ujumuishaji mataifa miaka 70 baada ya kuhusika na mmoja ya ukatili mbaya katika vita kuu vya pili vya dunia.

Lakini Ujerumani, taifa lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya lina kasoro moja kubwa: Kukosa kwake uwezo unaolingana na wa viongozi wenye malengo mjini Moscow na Beijing. Na kwa juhudi zake zote kansela wa Ujerumani Angela Merkel anakabiliwa na kampeni ngumu y akuchaguliwa tena mwaka huu, ambako atagundua iwapo Ujerumani ina kinga dhidi ya kitisho kipya cha siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia.

Mwandishi: Iddi Ssessanga

Mhariri: Daniel Gakuba