Nchi jirani na Korea kaskazini zapinga kuishambulia kijeshi nchi hiyo
10 Oktoba 2006Uchina na Korea ya kusini, zimepinga wazo la kuishmabulia kijeshi Korea ya kaskazini ambayo inalaumiwa kwa kuripua jana bomu la kinyuklia chini ya ardhi. Japan nayo inasema ni budi kusubiri yathibitishwe madai ya majaribio hayo kabla ya kuchukuwa hatua ya kuweka vikwazo.
Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limeanza leo kujadili mswada wa sheria wa Marekani kuhusu udhibiti wa mipango ya Korea ya kaskazini juu ya silaha za makombora na za kinyuklia. Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa mataifa, John Bolton, alikuwa na haya ya kuelezea:
´´Tumekuwa tukiilenga mipango ya silaha za balistiki, nyuklia, baioloji na kemikali za Korea ya kaskazini pamoja na shughuli zingine haramu ikiwa ni pamoja na kuuza madawa ya kulevya kupitia wanadiplomasia wake, kutengeneza salafu bandia za kigeni zenye thamani kama vile dola, yaani njia zote ambazo Korea ya kaskazini inatumia kupata salafu za thamani kuendeleza mipango yake ya silaha. Hayo ndiyo malengo yetu´´.
Rushia na Uchina zimeitolea mwito Korea ya kaskazini irejee kwenye meza ya mazungumzo yaliokwama na nchi 6. Wakati huo huo, aafisa moja wa Korea ya kaskazini ambae hakutajwa jina lake, ameliambia shirika la habari la Korea ya kusini la Yonhap, kwamba Korea ya kaskazini iko tayari kwa mazungumzo juu ya swala la silaha na vile vile iko tayari kuuacha mpango wake wa kinyuklia ikiwa Marekani itachukuwa hatua zinazostahili.
Wakati huo huo, Shirika la chakula duniani WFP, limesema litasimamisha misaada yake kwa Korea ya kaskazini mwezi Januari mwaka ujao ikiwa halitapata fedha zaidi.