Ndege ya abiria ya Azerbaijan yaanguka
25 Desemba 2024Kwa mujibu wa taarifa watu 62 walikuwemo kwenye ndege hiyo. Wizara ya afya imesema kwenye taarifa yake kwamba manusura 28 wamepelekwa katika hospitali ya mkoa na watu watano kati ya hao wamo katika wadi ya uangalizi wa wagonjwa mahututi.
Wizara ya dharura ya Kazakhstan imesema huenda watu 42 wamefariki katika ajali hiyo ya ndege ya shirika la ndege la Azerbaijan. Ndege hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka mji mkuu wa Azerbaijan , Baku kuelekea Grozny, ambao ni mji mkuu wa Jamhuri ya Urusi ya Chechnya. Video zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha wakati ndege ilipoanguka karibu na uwanja wa ndege wa Aktau.
Uwanja wa ndege wa Grozny uliripotiwa kufungwa kwa sababu ya ukungu, sababu ya ndege hiyo kulazimika Kwenda katika uwanja wa Makhach-kala, wa mji mkuu wa mkoa wa Dagestan. Chanzo cha ajali hiyo awali hakikufahamika.