1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ndege za Kenya zashambulia kambi za al Shabab

7 Aprili 2015

Kikosi cha anga cha Kenya kimeangamiza kambi mbili za al Shabab nchini Somalia katika hatua ya kwanza kubwa ya kijeshi kujibu mapigo ya shambulio la kundi hilo liliouwa wanafunzi 148 nchini Kenya wiki iliopita.

https://p.dw.com/p/1F3GW
Bendera ya Kenya.
Bendera ya Kenya.Picha: picture-alliance/dpa

Kundi la al Shabab limekanusha kwamba kambi zake zimeshambuliwa kwa kusema kwamba mabomu hayo yameangukia shambani.

Msemaji wa jeshi la Ulinzi la Kenya David Obonyo amesema Jumapili (Aprili 6) kwamba ndege za kivita za Kenya zimeshambulia kambi hizo zilioko mkoa wa Gedo unaopakana na Kenya.

Amesema picha walizopiga kutoka angani zinaonyesha kwamba kambi hizo zimeangamizwa kabisa juu ya kwamba imewawia vigumu kukadiria kiwango cha maafa kutokana na mawingu yaliyotanda angani.

Obonyo ameongeza kusema kwamba mashambulizi hayo ni sehemu ya mchakato wa kuzuwiya wapiganaji wa al Shabab kuvuka mpaka na kufanya mashambulizi yao nchini Kenya na kwamba utaendelea kutekelezwa.

Kujibu mapigo

Mashambulizi hayo yanakuja kufuatia onyo la Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwamba atalipiza kisasi kwa hatua kali kadri inavyowezekana dhidi ya shambulio la wanamgambo wa al Shabab la Alhamisi lililouwa takriban wanafunzi 148 wakati walipovamia Chuo Kikuu cha Garissa kilioko kama kilomita 200 kutoka mpaka wa Somalia.

Mwanajeshi wa Kenya nje ya Chuo Kikuu cha Garissa wakati kilipovamiwa.
Mwanajeshi wa Kenya nje ya Chuo Kikuu cha Garissa wakati kilipovamiwa.Picha: picture-alliance/dpa/EPA/Dai Kurokawa

Kundi hilo la wanamgambo lenye mafungamano la Al Qaeda limeuwa zaidi ya watu 400 katika ardhi ya Kenya katika kipindi cha miaka miwili iliopita wakiwemo 67 waliouwawa wakati wa kuzingirwa kwa jengo la maduka la Westgate mjini Nairobi hapo mwaka 2013.

Kenya imekuwa ikihangaika kuzuwiya kuingia kwa wanamgambo na silaha kwa kupitia mpaka wake na Somalia wenye urefu wa kilomita 700 na ghasia hizo pia zimekuwa zikiharibu uchumi wa nchi hiyo kwa kuwatia hofu watalii na wawekezaji kwenda Kenya.

Vikosi vya usalama lawamani

Msemaji wa operesheni za kijeshi wa al Shabab Abdasis Abu Musab amesema mojawapo ya kambi zake imeharibiwa katika mashambulizi ya Jumapili na kwamba mashambulizi hayo badala ya kushambulia kambi yameshambulia shamba.

Wanajeshi wa Kenya nje ya hospitali ya Garissa.
Wanajeshi wa Kenya nje ya hospitali ya Garissa.Picha: picture-alliance/dpa

Eneo la vijijini la Gedo nchini Somalia ni vigumu kufikiwa na habari juu ya mashambulizi hayo hazikuweza kuyakinishwa mara moja.

Kumekuwa na ongezeko la shutuma katika vyombo vya habari nchini Kenya kwamba taarifa muhimu za ujasusi zimepuuzwa na kwamba imechukuwa masaa saba kwa vikosi maalum vya usalama kufika katika chuo kikuu hicho kilioko kilomita 365 kutoka mji mkuu wa Nairobi.

Lakini vikosi vya usalama vimejitetea kwa namna ilivyokabiliana na shambulio hilo.

Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Amina Mohamed ameliambia shirika la habari la AFP kwamba "kupambana na ugaidi ni kama vile kuwa mlinda mlango wa timu.Unaokowa magoli 100 na hakuna mtu anayekumbuka.Wanakumbuka lile moja ulilofungwa."

Kenya yatakiwa kutowa vikosi Somalia

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye alikuwa waziri mkuu wakati Kenya ilipotuma wanajeshi wake nchini Somalia mwaka 2013 kupambana na al Shabab amesema serikali inapaswa kuanza kufikiria namna ya kujitowa nchini Somalia kama vile ilivyofanya Marekani kwa kuviondowa vikosi vyake baada ya wanajeshi wake 18 kuuwawa mjini Mogadishu mwaka 1993.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga.
Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga.Picha: DW/A. Schmidt

Odinga amekaririwa na gazeti la Kenya Standard la Jumapili akisema kwamba "Marekani ilikuwa na wanajeshi wengi nchini Somalia lakini iliwaondowa. Kenya pia inapaswa kuwaondowa wanajeshi wake kutoka Somalia."

Kenya hadi sasa haikuonyesha dalili yoyote ile kujitowa Somalia ambapo wanajeshi wake wakiwa sehemu ya kikosi cha Umoja wa Afrika wameyakombowa maeneo mengi yaliokuwa chini ya mikono ya al Shabab.

Hata hivyo wanadiplomasia wa nchi za magharibi wanasema kupoteza kwa maeneo hayo hakukudhofisha uwezo wa al Shabab kufanya mashambulizi ya kushtukiza nchni Somalia au nje ya nchi hiyo

Shambulio la Garissa ni baya kabisa kushuhudiwa katika ardhi ya Kenya tokea A Qaeda kuripuwa ubalozi wa Marekani mjini Nairobi hapo mwaka 1998 na kuuwa zaidi ya watu 200 na kujeruhi wengine maelfu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Sudi Mnette