1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Netanyahu akosolewa kwa lugha chafu dhidi ya Obama

27 Desemba 2016

Mwanadiplomasia wa zamani wa Marekani amesema lugha chafu inayotumiwa na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu baada ya Umoja wa Mataifa kushutumu ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Wayahudi haikubaliki.

https://p.dw.com/p/2Ut95
Israel Premierminister Netanyahu - Chanukka
Picha: Getty Images/AFP/J. Guez

"Lugha yenyewe inayotumiwa dhidi ya rais wa Marekani haijawahi kutokea, na haipaswi kuwa lugha inayotumiwa na mshirika kwa mshirika wake, hata akiwa amekasirishwa kivipi," Dan Kurtzer, ambaye alihudumu kama balozi wa Marekani nchini Israel chini ya utawala wa rais George W Bush aliiambia redio ya Israel.

Netanyahu amemtuhumu rais wa Marekani anaemaliza muda wake Barack Obama kwa kushinikiza kupitishwa kwa azimio hilo nyuma ya pazia. "Hatuna shaka kwamba utawala wa Obama ulilianzisha, kulisimamia na kuratibu maandishi yake na kushinikiza lipitishwe," alisema Netanyahu usiku wa Jumapili.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa lilipitisha azimio linalolaani makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina na kuitaka Israel kuyasimamisha, kwa kura 14 za kuunga mkono na kura moja ya kujizuwia ya Marekani.

Treffen Obama Netanjahu
Rais Barack Obama alipokutana na Netanyahu mjini New York Septemba 21, 2016.Picha: Reuters/K. Lamarque

Hatua za hasira

Netanyahu amechukuwa hatua kadhaa katika kujibu kile ambacho ofisi yake imekieleza kuwa ni azimio la "aibu" na la "kusikitisha." Amefuta ziara ya mwenzake kutoka Ukraine, ameitaka wizara ya mambo ya nje kuangalia upya uhusiano wa Israel na  taasisi za Umoja wa Mataifa na kumuita kwa mazungumzo balozi wa Marekani nchini humo.

Wawakilishi wa mataifa mengine yaliyopigia kura azimio hilo waliitwa pia katika wizara ya mambo ya nje siku ya Jumapili kujileleza. Vyombo vya habari vya ndani ya Israel viliripoti kuwa Netanyahu alifuta mkutano uliokuwa umepangwa kati yake na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May kandoni mwa mkutano wa kimataifa wa kiuchumi katika kisiwa cha Uswisi cha Davos mwezi ujao.

Naibu balozi wa Uingereza nchini Israel, Tony Kaye, ambaye alikuwa mmoja wa mabalozi walioitwa, aliiambia redio ya jeshi siku ya Jumatatu kwamba alivunjwa moyo kwamba Netanyahu hakutaka kuzungumza na na May, na kwamba alitaraji kutakuwepo na nafasi ya mazungumzo hayo siku za usoni.

Hofu ya kuchukiwa hatua zaidi

Kuna uvumi kwamba Netanyahu anawasiliana na utawala unaokuja wa Donald Trump na anahofia kwamba utawala wa sasa unapanga kuchukuwa hatua za ziada kabla ya Januari 20.

Westbank - Siedlung Ramat Shlomo
Ujenzi wa makaazi ya walowezi ukiendelea katika eneo la Ramat Shlomo Desemba 23, 2016, huku Jerusalem ikionekana kwa nyuma.Picha: picture-alliance/dpa/J. Hollander

Mkutano unapangwa kufanyika Januari 15 mjini Paris, Ufaransa kama sehemu ya juhudi za amani za Ufaransa, na vile vile fununu za hotuba ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry kuhusu vigezo vya suluhisho la mataifa mawili.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Avigdor Lieberman siku ya Jumatatu aliushambulia mkakati unaopangwa wa amani, akiutaja kama "mahaka dhidi ya Israel." Serikali ya Israel imekuwa ikikataa mara kwa mara juhudi za kuitisha mkutano wa kimataifa wa amani, wakati viongozi wa Palestina wanakaribisha mpango huo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae

Mhariri: Sekione Kitojo