NEW DELHI : India na Pakistan kujadili ugaidi
14 Novemba 2006Wanadiplomasia wa ngazi ya juu kutoka mahasimu wakubwa wawili India na Pakistan wameanza mazungumzo kwa mara ya kwanza karibu katika kipindi cha mwaka mzima ikiwa ni juhudi za kufufuwa mchakato wa amani ambao ulisistishwa kutokana na miripuko ya mabomu iliosababisha maafa mjini Mumbai hapo mwezi wa Julai.
Mazungumzo hayo ya siku mbili kati ya majirani hao wawili wenye kumiliki silaha za nuklea yanatazamiwa kuanzisha mfumo wa kupambana na ugaidi.
India ilisitisha mazunguzo na Pakistan baada ya kulilaumu shirika la ujasusi la Pakistan na Kundi la wanamgambo wa Kiislam kwa kuhusika na mirupuko hiyo ya mabomu ya Mumbai ambapo watu 186 waliuwawa na wengine 800 kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa wanadiplomasia mazungumzo hayo ya New Delhi pia yanatazamiwa kujadili kukomeshwa kwa mzozo juu ya Mto wa barafu wa Siachen ulioko Kashmir.
Lakini sio rahisi kufikiwa kwa maendeleo juu ya suala kutokana na kutokuwa tayari kwa jeshi la India kuondosha vikosi vyake kwa kile kinachonekana kuwa ni medani kubwa kabisa ya mapambano duniani.
India inaona kuondowa vikosi vyake katika mto huo wa barafu kutadhoofisha msimamo wake.