NEW YORK: Baraza la usalama lajadili vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini
11 Oktoba 2006Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linakutana leo kujadili vikwazo vitakavyowekewa Korea Kaskazini kwa kufanya jaribio la sihala ya kinyuklia.
Marekani na Japan zinataka hatua kali zichukuliwe dhidi ya Korea Kaskazini lakini China na Urusi zinaendelea kupinga kitisho cha hatua ya kijeshi.
Akizungumza juu ya mzozo wa Korea Kaskazini waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair amesema,
´Tofauti kati ya nchi kama Uingereza, au nchi kama India na Korea Kaskazini ni kwamba sisi ni nchi za kidemokrasia. Tunafuata sheria, tunaheshimu majukumu yetu ya kimataifa. Lakini Korea Kaskazini haifanyi lolote miongoni mwa mambo haya.´
Korea Kaskazini imeonya leo kwamba itavichukulia vikwazo vyovyote vikali dhidi yake kuwa tangazo la vita dhidi yake.
Naibu kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Yong Nam, amesema uamuzi wa kufanya majaribio zaidi utategemea hatua zitakazochukuliwa na Marekani.
Aidha kiongozi huyo amesema sera za Marekani kuelekea Korea Kaskazini ndizo zitakazoamua ikiwa nchi hiyo itarudi kwenye mazungumzo ya mataifa sita kuhusu mpango wake wa kinyuklia yaliyokwama.