NEW YORK: Baraza la usalama lakutana kujadili vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini
11 Oktoba 2006Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litakutana leo kujaribu kufikia makubaliano ya vikwazo vitakavyowekewa Korea Kaskazini kwa kufanya jaribio la sihala ya kinyuklia.
Marekani na Japan zinataka hatua kali zichukuliwe dhidi ya Korea Kaskazini lakini China na Urusi zinaendelea kupinga kitisho cha hatua ya kijeshi.
Akizungumza juu ya vikwazo hivyo balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, John Bolton alisema vikwazo havitahusu mahitaji muhimu.
´Vikwazo tunavyofikiria havilengi mahitaji ya kimsingi, ingawa tutakuwa na aina tofauti ya vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini kununua bidhaa zisizo muhimu kutoka mataifa ya kigeni ili kuidhoofisha serikali na mpango wake wa silaha.´
Naibu waziri wa mambo ya ndani wa Marekani, Christopher Hill amesema serikali ya Washington inataka hatua kali ichukuliwe na Umoja wa Mataifa.