New York. Korea ya kaskazini yawekewa vikwazo.
15 Oktoba 2006Baraza la usalama la umoja wa mataifa limepiga kura kwa kauli moja kuweka vikwazo vya kiuchumi na silaha dhidi ya Korea ya kaskazini kwa jaribio lake la silaha za kinuklia.
Azimio hilo lililotayarishwa na Marekani linazuwia biashara na Korea ya kaskazini itakayohusu silaha za hatari na pia limeweka vikwazo dhidi ya silaha kubwa za kivita pamoja na bidhaa ambazo si za lazima.
Balozi wa Korea ya kaskazini katika umoja wa mataifa , Pak Gil Yon , ametoa matamshi makali dhidi ya azimio hilo akiyashutumu mataifa wanachama wa umoja wa mataifa kwa kuwa kama genge la majambazi.
Rais wa Marekani George W. Bush amesema kuwa hatua hizo zinaonyesha kuwa dunia imeungana katika msimamo wake dhidi ya mipango ya silaha za kinuklia za Korea ya kaskazini.