1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK: Mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Marekani na Korea Kaskazini yafanyika

6 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCLp

Mazungumzo ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na Korea Kaskazini yatafanyika leo mjini New York Marekani kwa mara ya kwanza katika miaka 50.

Mkutano huo ni sehemu ya mkataba uliofikiwa mwezi uliopita kwenye mkutano uliofanyika mjini Beijing nchini China ambapo Korea Kaskazini ilikubali kuachana na sehemu ya mpango wake wa nyuklia.

Akizungumza juu ya mkutano huo, kiongozi wa shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za kinyuklia, Mohammed El Baradei, amesema, ´Lengo ni kuona vipi tunavyoweza kuirejesha Korea Kaskazini katika uhusiano wa kawaida na shirika la IAEA na kuona vipi wachunguzi wa shirika hili watakavyokwenda tena nchini humo. Kwa mujibu wa makubaliano ya mkutano wa Beijing, shughuli hii inatakiwa kukamilishwa katika kipindi cha siku sitini.´

Mkutano wa mjini New York unawaleta pamoja mpatanishi wa Marekani katika mzozo huo wa nyuklia, Christopher Hill, na mpatanishi wa Korea Kaskazini, Kim Kye-gwan, katika ubalozi wa Marekani kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Ajenda ya mkutano huo inatuwama juu ya madai ya Marekani kuitaja Korea Kaskazini kuwa taifa la kigaidi na uwezekano wa kuiondolea vikwazo. Mazungumzo na Marekani ni sharti lililowekwa na Korea Kaskazini kabla kuachana na mpango wake ya nyuklia.

Wachambuzi wanayaeleza mazungumzo hayo kuwa maendeleo mapya katika juhudi za kumaliza uhasama wa miaka mingi tangu Marekani ilipokiongoza kikosi cha kimataifa kuivamia Korea Kaskazini wakati wa vita vya Korea kati ya mwaka wa 1950 na 1953.