1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NGOZI/BURUNDI: Watoro wa mahakama za Gachacha hawatapewa vibali vya kuwa wakimbizi nchini Burundi

28 Aprili 2005
https://p.dw.com/p/CFIh

Maafisa nchini Burundi wamesema kwamba maelfu ya wahutu kutoka Rwanda wanaokimbilia nchini Burundi kwa hofu ya kushtakiwa kwenye mahakama za kienyeji maarufu Gachacha, kwa mauaji ya halaiki hawatapewa vibali vya ukimbizi nchini Burundi.

Uamuzi huo umekuja baada ya mkutano uliofanyika kaskazini mwa Burundi uliolenga kutuliza wasiwasi wa kidiplomasia kati ya Bujumbura na serikali ya Kigali juu ya kuhama kwa wahutu ambao serikali ya Rwanda inashikilia ni wakimbizi wanaokwepa sheria na hawapasi kupewa vibali vya kuwa wakimbizi.

Waziri wa usalama nchini Rwanda Salvator Ntihabose aliyeungoza ujumbe kutoka Bujumbura katika mkutano huo amesema kundi lake pamoja na ujumbe wa Rwanda waliamua kuunda kamati ya pamoja itakayowashawishi wahutu wanaokimbilia Burundi kurudi nchini mwao.

Rwanda imeikosoa serikali ya Burundi kwa kuwakubali wahutu wanaokimbilia nchini humo na kuishutumu kwa kuwatia moyo washukiwa kutoroka mashtaka yanayowakabili ya kuhusika katika mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini Rwanda.Takriban watu 5000 wamekimbilia Burundi kuanzia mapema mwezi huu kufuatia kufunguliwa kwa mahakama za Gachacha.