1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Njaa huenda ikazidi Sudan Kusini, UN

21 Aprili 2017

Watu laki moja nchini Sudan Kusini wanakabiliwa na ukosefu wa chakula wakati ambapo nchi hiyo ikizidi kuzongwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/2bfg2
Äthiopien Flüchtlinge aus Südsudan
Mtoto anayekabiliwa na utapia mlo katika hospitali moja Sudan KusiniPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Abbott

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sudan Kusini ameonya kuwa iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, hali ya ukame inaweza kuwa mbaya zaidi.

Maria Nyamuoka ana miaka 28 na anaishi katika jimbo la Unity. Ni mama mwenye watoto watatu na anasema, "watoto hulalamika kila mara kwamba wanahisi njaa, lakini sina cha kuwapa." Yungiyungi, majani pamoja na mizizi ndiyo inayowatenganisha watu wa Sudan Kusini na kifo baada ya kunaswa katika mapigano ya nchi hiyo yaliyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Huenda njaa ikaenea maeneo mengi nchini humo

Katika lugha ya Kinuer, yungiyungi huitwa "yiel", majani hayo hukaushwa na kupikwa lakini wazazi huko Sudan Kusini huwapa watoto wao mabichi ili kuyazima makali ya njaa. Familia nyingi hula jioni pekeyake kwa kuwa watoto hawawezi kulala wakiwa na njaa. Umoja wa mataifa ulitangaza rasmi kwamba kuna njaa katika baadhi ya sehemu za jimbo la Unity mwishoni mwa mwezi Februari, hiyo ikiwa ni njaa ya kwanza kutambulika rasmi ulimwengu mzima tangu mwaka 2011.

Südsudan Frauen mit Säcke in Nimini village
Wanawake wanabeba chakula cha msaada katika jimbo la Unity, Sudan KusiniPicha: Reuters/S. Modola

Stefano Temporin ni mkurugenzi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini anayehusika na masuala ya uratibu wa misaada, na anaonya, "iwapo jamii ya kimataifa haitoingilia kati na kutoa msaada sasa, njaa hii itaenea katika maeneo mengi nchini."

Kulingana na Umoja wa Mataifa, watu laki moja ni wahanga wa njaa wa moja kwa moja na milioni moja wengine wako katika hatari hiyo. Wa kwanza kuathirika hua ni watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, kutokana na kuwa na kinga dhaifu ya mwili. Jumla ya watu milioni 5.5 wanategemea chakula cha msaada nchini Sudan Kusini.

Njaa Sudan Kusini ni janga lililosababishwa na wanadamu

Kijiji cha Ganyiel ni kijiji maskini kilicho na nyumba za udongo zisizo na umeme, kijiji hicho hakina mtandao wa simu wala barabara zinazopitika na daktari mmoja pekeyake, ndiye anayewahudumia wakaazi 50,000 wanaoishi kijijini humo. Mashirika ya kutoa misaada yanashindwa kufika katika kijiji kama hiki kutokana na mapigano yanayoendelea, hivyo basi misaada wanayopata mara nyingi huangushwa kutumia helikopta.

Südsudan WFP Hilfe in Rubkuai
Ndege ya WFP ikiangusha misaada ya chakula katika jimbo la Unity, Sudan KusiniPicha: Reuters/S. Modola

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer, anaelezea hali hii ya njaa katika taifa hilo changa zaidi duniani, kama janga lililosababishwa na wanadamu, isipokuwa sehemu ndogo tu ya nchi hiyo inayokumbwa na ukame. Shearer anasema, aghalabu njaa nchini humo husababishwa na mapigano na cha muhimu kinachohitajika kufanywa ni kusitishwa kwa mapigano hayo.

Sudan Kusini iliyo na ukwasi wa mafuta ilipata uhuru wake mwaka 2011 kutoka Sudan, lakini mwishoni mwa mwaka 2013, kulizuka mzozo wa madaraka baina ya rais Salvar Kiir anayetokea kabila la Dinka na makamu wake Riek Machar wa kabila la Nuer.

Mwandishi: Jacob Safari/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga