1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya yanukia

31 Machi 2012

Michuano ya marudiano ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya itachezwa wiki ijayo. Bayern Munich italenga kuhakikisha kuwa inajikatia tiketi ya kucheza fainali katika uga wa nyumbani Allianz Arena.

https://p.dw.com/p/14V7i
Bayern Munich's Mario Gomez (C) celebrates with team mate after scoring a goal against Olympique Marseille during their quarter-final first leg Champions League soccer match at the Velodrome Stadium in Marseille, March 28, 2012. REUTERS/Philippe Laurenson (FRANCE - Tags: SPORT SOCCER)
Picha: Reuters

Magoli katika kila kipindi kutoka kwa Mario Gomez na Arjen Robben  siku ya Jumatano yaliipa Bayern Munich ya Ujerumani ushindi wa 2-0 dhidi ya Olympique Marseille. Ushindi huo umewaweka miamba hao wa ligi ya soka Ujerumani Bundesliga hatua moja karibu na nusu fainali ya kombe hilo la Mabingwa barani Ulaya maarufu kama UEFA Champions League.

Ushindi wa Bayern unawafanya kuwa timu inayopigiwa upatu kufuzu kwa nusu fainali dhidi ya Real Madrid ambao siku ya Jumanne walishinda magoli matatu wka sifuri nyumbani kwa APOEL Nicosia katika mechi y amkondo wa kwanza.

Akizungumza baada ya mchuano kocha Jupp Heynckes alisema kitu cha pekee ambacho hakikuwa kizuri kwao ni kwamba walipata kadi za njano. Moja ilimwendea mchezaji wa akiba Bastian Schweinsteiger ambaye sasa hatacheza katika mchuano wa marudiano. Naye Robben alisema wangali na mchuano mmoja wa kucheza nyumbani katika uwanja Allianz Arena kabla ya kusema wamefuzu kuingia nusu fainali.

Barcelona kutamba nyumbani

Ama mabingwa wa Ulaya Barcelona walitoka sare ya bila kufungana na viongozi wa ligi ya soka Italia Serie A AC Milan uwanjani San Siro na kuwacha nafasi ya robo fainali hiyo kuwa  kuwa wazi na amashabiki wakiendelea kujiuliza nani atafuzu  kuingia nusu fainali

Barcelona watalenga kung'ara katika uwanja wao wa nyumbani Camp Nou, Uhispania
Barcelona watalenga kung'ara katika uwanja wao wa nyumbani Camp Nou, UhispaniaPicha: Reuters

Barcelona waliumiliki mpira kwa kiwango kikubwa lakini walikuwa na matatizo ya kufanya mashambulizi yoyote katika lango la adui Milan ambao walikuwa wamejpanga vyema katika safu yake ya ulinzi, hadi dakika za mwisho wakati vijana hao wa kocha Pep Guardiola walipokaribia mara mbili kupata bao.

Kipa wa Barca Victor Valdes amesema walikuwa na nafasi nyingi lakini hawakuzitumia vyema. Kwamba walijaribu kupokezana pasi fupi wakati wakiumiliki mpira kwa muda mrefu. Anasema mchuano bado ni wazi na sasa utaamuliwa  kwao nyumbani mjini Barcelona.

Klabu ya Chelsea imesema iko tayari kumlipa Kocha wa Ufaransa Laurent Blanc mshahara wa pauni milioni 8 kwa mwaka, ambao utamfanya we kocha anayelipwa zaidi nchini Uingereza kama atakubali kujiunga na klabu hiyo baada ya mashindano ya kombe la Ulaya.

Gazeti la Times liliripoti siku ya Jumanne kuwa mawakala wa Chelsea wamemuarifu mmiliki wa Klabu hiyo Roman Abromovich kuwa wamefanya mawasiliano na kambi ya kocha huyo kujua kama ana nia ya kubeba mikoba ya kuinoa klabu hiyo.

Gazeti hilo liliripoti kuwa Abromovich alikuwa tayari kutoa kiasi cha pesa kitakachomfanya kocha huyo awe anayelipwa zaidi na kumpiku Kocha wa Manchester Cíty Roberto Mancini anayelipwa mshahara wa pauni milioni 5.

Kaimu Mkufunzi wa Chelsea Roberto di Matteo amesajili matokeo bora
Kaimu Mkufunzi wa Chelsea Roberto di Matteo amesajili matokeo boraPicha: AP

Chelsea inayokabiliana na kibarua cha kucheza na Benfica katika robo fainali ya michuano ya Mabingwa wa Ulaya siku ya Jumanne inanolewa kwa sasa na kocha wa muda Roberto Di Matteo kufuatia kutimuliwa kwa Mreno Andre-Villa Boas mwanzoni mwa mwezi huu.

Fainali ya kombe la Italia

Nchini Italia, uwanja itakapofanyika fainali ya kombe la Italia kati ya Juventus na Napoli hapo Mei 20 bado haujajulikana baada ya kutokea mzozo kati ya Kamati ya Olimpiki ya Italia na wa wasimamizi wa ligi ya mpira wa miguu Serie A juu ya matumizi ya Uwanja wa Stadio Olimpico mjini Roma.

Siku ya Jumatano  viongozi wa ligi kuu nchini humo walipitisha uamuzi wa kuchezea fainali hizo jijini Roma lakini Gianni Petrucci, Mkuu wa Kamati ya Olimpiki ambao ndiyo wamiliki wa uwanja wa Olimpico alikasirika kwa sababu Seria A hawakumuomba ruksa ya kuutumia na hivyo kuamua kuzuia matumizi yake, huku akisisitza kuwa mjadala huo umefungwa na itawabidi Seria A watafute uwanja mwingine. Klabu ya Juventus ilikasirishwa na uamuzi huo na kusema kuwa mechi kubwa kama hiyo inapaswa kuchezewa katika uwanja maarufu katika mji mkuu wakati mashabiki wa Napoli hawataki kusafiri kwenda uwanja wa Milan, Sansiro.

Mchezaji muhimu wa mabingwa wa Ujerumani Borrusia Dortmund mario Goetze ameongeza mkataba wake na klabu hiyo kwa miaka miwili hadi 2016 na kuzima fununu za kuwepo uwezekano wa yeye kuhamia katika moja klabu kubwa barani Ulaya.

Mario Götze alihusishwa na uvumi wa kuhamia klabu ya Arsenal nchini Uingereza
Mario Götze alihusishwa na uvumi wa kuhamia klabu ya Arsenal nchini UingerezaPicha: picture alliance/dpa

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 19 amekuwa klabuni hapo kwa muongo mzima na amekuwa akiviziwa na klabu kubwa barani ulaya zikiwemo Arsenal, na nyingine kutoka Hispania na Uigereza.

Kila mmoja anafahamu ni jinsi gani nikiwa Dortmund, alisema Goetze ambaye yuko mbioni kurejea uwanjani baada ya kuwa majeruhi kwa zaidi ya miezi miwili. Borrusia wako mbioni kutwaa ubingwa wa ligi ya Ujerumani kwa mara ya pili mfululizo na wanaongoza msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi tano zaidi ya Bayern München inayoshika nafasi ya pili.

Mwanafunzi atupwa jela kufuatia uchochezi Twitter

Mwanafunzi  mmoja wa  biolojia nchini Uingereza amehukumiwa kwenda jela kwa siku 56 na mahakama ya wilaya nchini humo kwa kosa la kutoa maneno ya uchochezi kupitia mtandao wa kijamii wa twitter, kuhusiana na mchezaji wa Bolton Fabrice Muamba.

Muamba anaendelea kupata nafuu baada ya kupata mshtuko wa moyo wakati wa mechi ya kombe la  FA Machi 17 ambapo Liam Stacey anadaiwa kutoa maneno kadhaa kupita mtandao wa Twitter. baada ya malalamiko kutoka kwa umma Stacey alikamatwa na kukiri siku ya jumanna kuwa alitenda kosa la uchochezi wa ubaguzi wa rangi.

Mtayarishaji: Mohammed Abdul-Rahman

Mhariri: Mohamed Khelef