Obama abanwa mbavu na mapinduzi ya Waarabu
14 Machi 2011Haijawahi kutokezea, tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia, kwa rais wa Marekani kujikuta akikabiliana na changamoto nyingi na ukosefu wa uhakika panapohusika sera ya nje ya taifa hilo kuelekea eneo muhimu kisiasa na kimkakati na kwa wakati mmoja.
Lakini hiyo ndiyo hali ilivyo sasa kwa Rais Barack Obama, ambaye anaongoza taifa lake katika wakati ambao karibu eneo zima la Mashariki ya Kati, Ghuba na Uarabuni linakumbwa na vuguvugu la umma, linaloziondoa tawala kongwe madarakani.
Utawala wa Rais Barack Obama umeelemewa na mengi mwaka huu: Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya, migogoro ya kisiasa inayokua kila siku nchini Bahrain, Yemen, Jordan, Oman na Saudi Arabia. Wote hawa ni washirika wa Marekani.
Kisha kuna wasiwasi wa hatima ya Misri, kwamba kipindi cha sasa cha mpito, kisije kumalizikia kwa serikali kuangukia mikononi mwa watu wenye sera za kiuhasama dhidi ya Israel.
Hata Rais George Bush (Mkubwa) alikumbana na hali kama hii wakati wa kile kinachoitwa "Mapinduzi ya mwaka 1989" yaliyoziondoa tawala za kikomunisti katika Ulaya ya Mashariki na kuuporomoa Umoja wa Kisovieti.
Lakini matukio haya hayakutokezea kwa pamoja, na hivyo yaliwawezesha watunga sera kushughulika na mgogoro mmoja kwa wakati mmoja.
Vile vile, historia ya zaidi ya miaka 40 ya Washington kufanya kazi na makundi ya wapinzani katika Ulaya ya Mashariki, ilimuwezesha Rais Bush kufanya kazi akiwa na imani kuwa, mageuzi haya yangeliekea kule Marekani inakotaka.
Lakini kadiri Rais Obama anayojiona kuufanyia kazi upande sahihi wa historia, ndivyo anavyojikuta akikosa uhakika ikiwa vuguvugu hili la ghafla katika nchi za Uarabuni litakidhi matakwa ya Marekani.
Miongoni mwa sababu za wasiwasi huu, ni ukweli kuwa historia ya taifa hilo katika eneo hili ni ya kuudhi, tafauti na ile ya zama za Vita Baridi kwenye nchi za Ulaya Mashariki na hata kwa uliokuwa Umoja wa Kisovieti.
bTabia ya Marekani kuwaunga mkono watawala wa kidikteta katika eno hilo na kuibeba Israel, imeupekelea umma wa Kiarabu kuwa na shaka zaidi na dhamira ya Washington kuliko vile watu wa Ulaya ya Mashariki walivyokuwa miaka 20 iliyopita.
Pia, kuwepo wanajeshi wake 50,000 nchini Iraq na wengine 100,000 nchini Afghanistan, kunazifanya kumbukumbu za machungu ya uvamizi wa taifa hilo kwenye ardhi za eneo hilo kutokusahaulika haraka.
Wakati vuguvugu lilipoanza Tunisia na Misri, ajenda kuu za Washington zilikuwa ni Iraq, Afghanistan, uhusiano wake unaoyumba na Pakistan na mpango wa nyuklia wa Iran.
Kwa siku za karibuni, hata hivyo, ni kama kwamba ajenda imeelekezwa kwengine.
Marekani inapaswa kuwa imeshaondosha wanajeshi wake waliobakia Iraq, kufikia mwishoni mwa mwaka huu, lakini Waziri Mkuu Nouri al-Maliki ameenza kuwa na tabia za kidikteta, huku adui wake mkubwa, Ayad Alawi, wa muungano wa Iraqiya, akionekana kuja juu.
Fujo za wiki iliyopita kufuatia maandamano, ziliwafanya wachunguzi wahitimishe kuwa bado Iraq haijawa.
Afghanistan nako, ushindi wa majeshi ya Marekani dhidi ya Taliban unaonekana kuwa si wa kudumu. Hasa kwa kuwa yale mambo, ambayo mkuu wa operesheni ya Marekani huko, Jenerali David Petraeus, anasema ni muhimu, kama vile kupunguza ufisadi serikali, kufikisha huduma muhimu kwa watu, na kuongeza ufanisi wa jeshi la Afghanistan, hayaonekani kupata maendeleo makubwa.
Pia kuna hali ya kutoaminiana baina ya Rais Hamid Karzai na utawala wa Washington, hasa kwa sababu ya kuongezeka kwa mashambulizi ya Marekani, ambayo kimakosa yanaua raia wa kawaida.
Mambo yote haya yakitiwa kwenye kapu moja la sera za nje, mtu anaweza kukisia zigo ambalo Rais Obama limemuelemea mabegani mwake.
Mwandishi: Mohammed Khelef/IPS
Mhariri: Josephat Charo