1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Odinga ana matumaini ya ushindi.

26 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CgIB

Nairobi.

Mgombea wa upinzani nchini Kenya jana Jumanne ameeleza matumaini yake ya ushindi katika uchaguzi wa rais ambao nguvu za wagombea zinaonekana kuwa karibu sawa, licha ya madai mapya ya wizi wa kura kujitokeza siku mbili kabla ya uchaguzi.

Raila Odinga mwenye umri wa miaka 62, mwanasiasa ambaye aliwahi kuwekwa kizuizini na ambaye anaongoza katika maoni ya wapiga kura amesema kuwa anamatumaini ya kupata kura zinazotaka mabadiliko, katika uchaguzi wa hapo Alhamis.

Odinga amesema kuwa amefanya kila ambalo linawezekana kwa binadamu katika kampeni hizo mbali ya vipingamizi kadha vilivyokuwapo. Kwa hiyo amesema anamatumaini makubwa kuwa wapiga kura nchini humo watapiga kura kwa ajili ya mabadiliko.

Wakati huo huo maelfu ya makarani wa uchaguzi nchini humo wameandamana wakitaka kuongezwa mshahara wa shilingi 700 kiasi cha dola 11 kwa siku na kutishia kutofanyakazi katika siku ya uchaguzi.

Rais Kibaki wakati huo huo alihudhuria misa katika kanisa Katoliki katika mji mkuu wa Nairobi , na kisha kuondoka bila kusema lolote, lakini kadinali John Njue amewaambia wapiga kura wote waliojiandikisha wapige kura kwa busara kwa ajili ya viongozi ambao watawatumikia kwa muda wa miaka mitano ijayo.