1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Odinga kurejea Cote d'Ivoire wiki hii

11 Januari 2011

Ziara yake ni juhudi ya hivi karibuni kujaribu kumshawishi rais Gbagbo aondoke madarakani na kumkabidhi mpinzani wake Alassane Ouattara.

https://p.dw.com/p/zwMA
Raila Odinga, kulia, na Alassane OuattaraPicha: AP

Mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mzozo wa Cote d´Ivoire, Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga anatarajiwa kurudi katika taifa hilo la Afrika Magharibi baadae wiki hii. Msemaji wa Bwana Odinga, Dennis Onyango aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP, huenda mpatanishi huyo akarejaea Cote d'Ivoire Alhamisi au Ijumaa. Kwa mujibu wa msemaji huyo, Bwana Odinga atakutana kwanza na kumuarifu Kamishna wa Umoja wa Afrika, Jean Ping mjini Nairobi kesho Jumatano kabla ya kuelekea Cote d'Ivoire.

Ziara ya kwanza ya Odinga Abidjan tangu alipoteuliwa na Umoja wa Afrika kama mpatanishi wa mzozo wa kisiasa ilimalizika tarehe 5 ya mwezi huu wa Januari, huku kukiwa na maendeleo kidogo katika kuutatua mzozo huo ambao umeirejesha Cote d'Ivoire katika uwezekano wa kuzuka tena vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Waziri huyo mkuu wa Kenya, amesema Rais Laurent Gbagbo alikubali kuondoa kizuizi katika hoteli inayotumiwa kama makao makuu ya mpinzani wake Alassane Ouattara, lakini hayo hayakufanyika. Katika ziara yake ya awali Odinga alisema Gbagbo hatofunguliwa mashtaka iwapo atakubali kumtambua Ouattara kama rais halali wa nchi hiyo na kuachia madaraka kwa amani.