1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ofisi ya Merkel kushughulikia wakimbizi

Admin.WagnerD7 Oktoba 2015

Katika juhudi za kutuliza wasiwasi wa wajerumani juu ya wimbi la wakimbizi , baraza la mawaziri la nchi hiyo limempa mkuu wa ofisi ya Kansela Angela Merkel Peter Altmaier jukumu la kulishughulikia suala hilo.

https://p.dw.com/p/1Gk5R
Kiongozi wa Ofisi ya Kansela Merkel, Peter Altmaier
Kiongozi wa Ofisi ya Kansela Merkel, Peter AltmaierPicha: picture-alliance/dpa/S. Kahnert

Tangazo la msemaji wa Serikali mjini Berlin Georg Streiter ambalo limetolewa baada ya kikao cha baraza la mawaziri leo hii limesema Peter Altmaier atawianisha na kuimarisha shughuli za wizara zinazohusika na kuwapokea na kuwapa hifadhi wakimbizi nchini Ujerumani.

Ujerumani imekuwa kimbilio la wahamiaji wengi wanaokimbia vita nchini Syria na Afghanistan. Mwezi uliopita Kansela Angela Merkel alisema kwamba Ujerumani itapata njia ya kuwashughulikia wakimbizi wanaomiminika nchini humo, lakini wingi wa wakimbizi hao, ambao baadhi ya ripoti zinasema ni kati ya watu milioni 1 na milioni 1.5, imewashtua wajerumani, ambao wengi wao hapo awali walimuunga mkono kwa dhadi Bi Merkel.

Kitu kingine kinachozidisha wasiwasi wa wajerumani, ni dhana kwamba wengi wa hao wanaoingia nchini humo sio wakimbizi wa kweli, bali ni wahamiaji wa kiuchumi ambao wametumia fursa ya wimbi hili kujipenyeza.

De Maiziere ''hakutengwa''

Msaidizi wa Peter Altmaier atakuwa Helge Braun, ambaye kawaida ni mratibu wa shughuli za serikali kuu na zile za majimbo, ambaye ataongoza kitengo maalum cha masuala ya wakimbizi.

Umaarufu wa Kansela Merkel umeshuka kutokana na jinsi alivyolishughulikia suala la wakimbizi
Umaarufu wa Kansela Merkel umeshuka kutokana na jinsi alivyolishughulikia suala la wakimbiziPicha: Reuters/A. Schmidt

Watu walio karibu na Kansela Angela Merkel wamesema hatua hiyo sio kumtenga waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere, ambaye hivi karibuni amekosolewa kushindwa kulishughulikia ipasavyo wimbi hilo la wakimbizi. Watu hao wanasema lengo la hatua hiyo ni kuipunguzia mzigo wizara yake.

Kansela Merkel anatarajiwa kushiriki katika kipindi maarufu baadaye leo, ambacho kinaoongozwa na Anne Will. Inafikiriwa kwamba mada kubwa itakuwa kuhusu wimbi hilo la wakimbizi, ambalo limedidimiza umaarufu wake miongoni mwa wajerumani.

Umaarufu wa Merkel katika mtihani

Ripoti ya kura ya maoni iliyochapishwa Jumatatu wiki hii imeonyesha kwamba asilimia 59 ya walioulizwa wanaamini kwamba uamuzi wa Bi Merkel kuwaruhusu wakimbizi kuingia nchini Ujerumani bila kusajiliwa, ulikuwa ni kosa.

Wingi wa wakimbizi wanaoingia Ujerumani umezusha wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wajerumani
Wingi wa wakimbizi wanaoingia Ujerumani umezusha wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wajerumaniPicha: picture alliance/AA/L. Barth

Kabla ya hapo lakini Kansela Merkel amekwenda katika bunge la Ulaya akiambatana na rais wa Ufaransa Francois Hollande, katika kikao ambamo yumkini suala la wakimbizi likajadiliwa.

Wakati huo huo maandamano yanatarajiwa kufanyika leo katika mji wa mashariki mwa Ujerumani wa Erfurt. Maandamano hayo yameandaliwa na chama kidogo kiitwacho Mbadala kwa Ujerumani, AfD, ambacho kiliundwa kikiwa na sera za kupinga Umoja wa Ulaya, ambacho sasa kimechukua msimamo mkali dhidi ya wahamiaji, tangu kutokea mpasuko ndani ya chama hicho mapema mwaka huu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/dpae

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman