Ongezeko la imani ya wanachi kwa vyombo vya habari Kenya
21 Desemba 2020Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2020 ya Baraza la vyombo vya habari nchini Kenya MCK, asilimia 97 ya raia nchini Kenya wana amini zaidi na vyombo vya habari hii ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na asilimia 91 mwaka jana huku ikibainika kuwa asilimia 55 ya walioshiriki kwenye utafiti huo wakisema wamekuwa wakitumia zaidi kwa kuona na kusikiliza vyombo vya habari pakubwa wakati huu wa janga la korona.
Soma pia: Kenya yatangaza hatua mpya za kupambana na corona
Afisa mkuu mtendaji wa baraza la vyombo vya habari David Omwoyo Omwoyo anasema wakenya wengi walitegemea sana vyombo vya habari kuwapa maelezo ya kina kuhusiana na hali halisi ya korona huku utegemezi wa televisheni ukipiku radio kwa kiasi cha hadi asilimia 47 ikilinganishwa na asilimia 34 katika matumizi ya radio, ila vyombo hivi ndivyo vinatumiwa na kutegemewa zaidi na wananchi.
Mkurugenzi wa kampuni ya utafiti nchini Kenya ya InfoTrack Angela Ambitho anasema utafiti huo ulihusisha wakenya 3074 katika maeneo yote nchini Kenya washirika wakiwa ni wenye umri wa miaka 18 na zaidi.
Mafanikio yashuhudiwa licha ya athari za Covid-19
Ambitho amesema ni wazi kuwa licha ya changamoto ambazo zimekumba sekta ya uandishi nchini utafiti huu unaonyesha bayana mafanikio pia yameshuhudiwa.
"Watu wachache wanafanya kazi na umoja wa kuendesha kazi kwa ubunifu na mafanikio mmeweza kuimarisha imani yenu kwa wananchi ikizingatiwa ongezeko la kutoka asilimia 24 hadi 35 nadhani kutokana na wengi kukaa nyumbani hasaa mwanzoni mwa janaga". Amesema Ambitho.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa baraza la vyombo vya habari (MCK) Maina Muiruri anasema ni kweli mapato ya vyombo vya habari yamepungua ila ni vyema kwa wakuu wa vyombo hivi wafahamu umuhimu wa hasaa kitengo cha habari na wawe tayari kukiimarisha katika kila hali ikizingatiwa idadi kubwa ya wakenya wanaotegemea na kufuatilia habari.
Katika utafiti huo, mitandao ya kijamii ambayo inaushawishi mkubwa nchini Kenya ni WhatsApp na Facebook huku kiwango cha wanaosoma magazeti kikishuka hadi asilimia 25.