Padri atekwa nyara na polisi DRC
3 Februari 2018Katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo polisi inatajwa kumteka nyara padiri hii leo baada ya misa ya Jumamosi mjini Kinshasa.Hayo yameelezwa na walioshuhudia wakati nchi hiyo ikiwa katika wasiwasi na mvutano mkubwa baina ya kanisa na serikali kuhusiana na hatua ya rais Kabila ya kukataa kuondoka madarakani.
Padri Sebastien alichukuliwa mateka na polisi muda mfupi baada ya kumalizika misa mtawa wa kanisa la parokia ya Mtakatifu Robert aliwaeleza waandishi habari wa shirika la AFP katika mji wa Nsele mashariki mwa mji mkuu Kinshasa. Gari ya polisi ilionekana katika maeneo ya kanisa hjilo na maafisa kadhaa kuteremka kwenye gari na kuanza kumpiga padri huyo alisikika akieleza mtawa mwingine ambaye pia alishuhudia tukio hilo.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa maafisa hao wa polisi walimsukuma padri huyo na kumuingiza ndari ya gari aina ya Jeep na kuondoka nae huku ikielezwa na watawa hao kwamba alikuweko mtu wasiyemfahamu aliyekuwa akichukua vidio ya padri huyo kupitia simu ya mkononi wakati misa ilipokuwa ikiendelea. Hata hivyo polisi imekataa kutoa maelezo yoyote hadi wakati huu kuhusu kisa hicho baada ya kutafutwa na AFP. Padri Sebastian Yebo amefanya kazi katika parokia ya hiyo tangu mwezi Agosti mwaka 2017.
Tukio hilo limetokea katika wakati ambapo ni baada ya kuchukuliwa hatua kali na serikali za kuwaandama waumini wakikatoliki kufuatia maandamano yaliyopangwa na kanisa hilo dhidi ya rais Kabila. Kiasi watu 15 wameuwawa kufikia sasa kutokana na hatua hiyo ya vikosi vya usalama iliyoshuhudiwa Desemba 31 na Januari 21 kwa mujibu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo Monusco.
Rais Kabila mwenye umri wa miaka 46 amekuwa madarakani toka mwaka 2001 chini ya serikali ambayo inakosolewa kwa ufisadi,ukandamizaji na uzembe.Muda wake kwa mujibu wa katiba ulimalizika Desemba mwaka 2016 lakini ameendelea kubakia madarakani hali ambayo inasababisha umwagikaji damu katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo:
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri Isaac Gamba