Papa Fransisko ahubiri kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe
15 Machi 2013Matamshi hayo ameyatoa katika mahubiri yake wakati wa Ibada ya Misa Takatifu na Makardinali waliomchagua, kwenye Kanisa dogo la Sistine mjini Vatican. Akihubiri katika Ibada yake ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki duniani, lenye Wakatoliki bilioni 1.2, Baba Mtakatifu Fransisko, amewataka Wakatoliki kuwa na ujasiri wa kutembea katika uwepo wa Yesu. Aidha, amewaonya Makardinali dhidi ya ulimwengu wa kiibilisi. Amesema mtu akimfuata Kristo bila Msalaba hawezi kuwa mfuasi wa kweli na badala yake anakuwa mwana wa ulimwengu huu, mfuasi wa ibilisi.
Siku yake ya kwanza kazini
Baba Mtakatifu alianza siku yake ya kwanza kazini jana Alhamisi, kwa kufanya maombi binafsi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Maggiore, mjini Roma. Aidha, alikutana na watu mjini Roma, pamoja na kuweka maua katika Goroto la Mama Bikira Maria katika Kanisa Kuu. Pia alisali katika altare (madhabahu) ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, mwanzilishi wa Shirika la Mapadri la Kijesuiti, shirika ambalo anatokea. Kisha Papa huyo mpya alikwenda kuchukua mizigo yake kutoka chumba cha wageni katikati ya Roma, ambako aliishi kabla ya kuanza kikao cha faragha cha baraza la Makardinali kupiga kura.
Siku yake ya pili kazini
Katika siku yake ya pili kazini, baadae leo Baba Mtakatifu Fransisko anatarajiwa kukutana na Makardinali wote walioko mjini Vatican. Aidha, taarifa kutoka Vatican zinaeleza kuwa kiongozi huyo mpya wa Kanisa Katoliki atakutana na Papa mstaafu, Benedikto wa Kumi na Sita siku chache zijazo. Baba Mtakatifu atasimikwa rasmi Jumanne ijayo ambapo itakuwa ni siku ya Mtakatifu Yosefu, ambaye ni Mtakatifu mlezi wa Kanisa mahalia na kuchukua nafasi ya Papa Benedikto wa Kumi na Sita aliyejiuzulu Februari 28, mwaka huu. Baba Mtakatifu Fransisko mwenye umri wa miaka 76, anakabiliwa na changamoto zinazolikumba Kanisa Katoliki katika majukumu yake mapya.
Taarifa kutoka Vatican zinaeleza kuwa baada ya kuchaguliwa siku ya Jumatano, Baba Mtakatifu Fransisko hakupanda gari la kifahari maalum kwa ajili ya Papa aina ya Limousine na badala yake alipanda basi pamoja na Makardinali wenzake. Akiwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires, aliishi kwenye nyumba ya kawaida na alikuwa akipanda basi kuelekea kazini.
Rais wa Taiwan kuhudhuria Ibada ya kusimikwa Papa
Wakati huo huo, Rais wa Taiwan, Ma Ying-Jeou anapanga kuzuru Vatican kuhudhuria Ibada ya Misa ya kusimikwa Baba Mtakatifu Fransisko. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Taiwan, Vanessa Shih amewaambia waandishi wa habari kuwa taarifa zaidi kuhusu ziara hiyo, zitatolewa baadae leo. Hata hivyo maafisa wanasema ziara hiyo ina lengo la kuikasirisha China.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Gakuba Daniel