SiasaMarekani
Pence awasilisha nyaraka za kuwania urais 2024
6 Juni 2023Matangazo
Makamu wa Rais wa zamani wa Marekani Mike Pence amewasilisha nyaraka zake katika Tume ya Uchaguzi na kujitosa rasmi katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais. Pence anatarajiwa kutangaza nia yake ya kugombea urais hapo kesho. Mrepublican huyo mwenye umri wa miaka 63 anampinga bosi wake wa zamani Donald Trump katika kinyang'anyiro cha uteuzi wa chama. Pence alikuwa naibu wake kuanzia mwaka wa 2017 hadi alipoondoka Ikulu ya White House kufuatia kushindwa kwake katika mwaka wa 2020. Kwa miaka mingi, Pence alikuwa mtiifu kwa Trump, lakini katika misukosuko iliyofuatia uchaguzi wa rais wa 2020, uhusiano wao ukaharibika.