Platini apoteza katika kesi yake ya rufaa
11 Desemba 2015Mahakama hiyo imesema kufanya hivyo kutakuwa ni kukiuka vizuizi vya kisheria na hakutompatia haki mtuhumiwa. Matthieu Reeb ni Katibu Mkuu wa Mahakama hiyo "Lengo la amri hii pia ni kuulinda uchaguzi wa rais wa FIFA, kwa sababu bila shaka utahitaji kuwa mchakato unaomhusu Michel Platini na wagombea wengine ukamilike kabla ya Februari 26, kabla ya uchaguzi huo, ili kuepusha utata utakaofuata kwa ombi la kufutwa uchaguzi wa rais. Hivyo amri ni kuzifunga kesi hizi kabla ya Februari 26, 2016"
Jopo la mahakama hiyo inayoshughulikia utatuzi wa migogoro katika michezo - CAS, limeacha muda wa sasa ubakie kama ulivyo likisema kwamba hali inaweza kubadilika ikiwa FIFA itarefusha kipindi cha kumsimamisha Platini kwa muda wowote zaidi ya siku 45, kwa kile kilichotajwa kuwa ni mazingira yasio ya kawaida. Platini alisimamishwa kufuatia uchunguzi unaoendelea kuhusu rushwa, akidaiwa alipokea kitita cha fedha kutoka kwa aliyekuwa Rais wa FIFA Joseph Blatter.
Hukumu ya jana ina maana kuwa matumaini pekee ya ya kweli kwa Platini kujitosa tena katika kinyang'anyiro cha urais wa FIFA ni ikiwa atapatikana bila makosa na Kamati ya Maadili ya FIFA itakapotoa uamuzi wake wa mwisho kwenye kesi hiyo unaotarajiwa kutolewa kabla ya Krismasi. Matthieu Reeb anaeleza "Jopo hili pia limezingatia kwamba kuwa sehemu ya uchaguzi wa rais, basi ilikuwa muhimu kwa Platini kufika mbele kamati ya uchaguzi ya FIFA ili kuidhinishwa nia yake ya kugombea, na ni kama haiwezekani, kwa mujibu wa jopo hili kuwa idhini ya aina hiyo inaweza kutolewa kabla ya uamuzi wa mwisho wa Kamati ya Maadili kufikiwa".
Kwa upande mwingine, uamuzi huo unaweza kusababisha Platini na Blatter kupigwa marufuku ya miaka kadhaa ikiwa watapatikana na hatia ya kufanya uovu wowote.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Iddi Sessanga