Platini kujiuzulu kuwa rais wa UEFA
10 Mei 2016Michel Platini atajiuzulu kuwa rais wa shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA baada ya mahakama ya upatanishi katika michezo CAS kuamua kukubali aendelee na adhabu yake ya kupigwa marufuku kujihusisha na shughuli za uongozi wa michezo, lakini adhabu hiyo imepunguzwa kutoka miaka sita hadi miaka minne.
Platini mwenye umri wa miaka 60 mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa , atawasilisha barua yake ya kujiuzulu katika mkutano mkuu wa shirikisho hilo, wamesema mawakili wake katika taarifa. Platini amesema uamuzi huo ulikuwa ukiukaji mkubwa wa haki, na ataendelea kutafuta haki yake katika mahakama za Uswisi.
Kifo cha mchezaji wa Cameroon
Wizara ya mambo ya ndani ya Romania imesitisha leseni ya kampuni ya binafsi ya magari ya kubebea wagonjwa ambayo ilimsafirisha mchezaji wa kati wa Dinamo Bucharest na timu ya taifa ya Cameroon Patrick Ekeng kwenda hospitali baada ya kuzimia uwanjani siku ya Ijumaa. Alifariki baadaye hospitalini.
Wizara hiyo imesema katika taarifa kwamba iligundua vifaa vya kumsaidia mgonjwa kupumua vikiwa bateri zake zimekwisha muda wake katika baadhi ya magari ya kubebea wagonjwa ya kampuni hiyo, na madawa yaliyotumiwa kumsadia mchezaji huyo kuweza kupumua yamekwisha muda wake.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Iddi sessanga