1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yawatawanya waandamanaji katika jiji la Kinshasa

Zainab Aziz Mhariri: Sudi Mnette
30 Juni 2019

Polisi katika mji mkuu wa Kinshasa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo wametumia mabomu ya kutoa machozi ili kuyavunja maandamano yaliyoandaliwa na upande wa upinzani.

https://p.dw.com/p/3LMXS
DR Kongo Unterstützer von Martin Fayulu in Kinshasa
Picha: Reuters/K. Katombe

Polisi pia waliizuia gari iliyokuwemo mgombea wa urais katika uchaguzi uliomalizika Martin Fayulu. Kiongozi mwingine wa upinzani, Adolphe Muzito, aliyekuwa waziri mkuu wa zamani pia alikuwemo ndani ya gari iliyombeba Martin Fayulu. Maafisa wa polisi wapatao 50 waliizunguka gari hiyo katikati ya barabara kuu ya Boulevard Lumumba.

Viongozi hao wawili walitoka kwenye gari kuzungumza na mkuu wa polisi wa Kinshasa Sylvano Kasongo huku waandamanaji wakiwa wamewazunguka.

Kiongozi wa upinzani nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Martin Fayulu
Kiongozi wa upinzani nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Martin FayuluPicha: Reuters/B. Ratner

Siku ya Jumamosi, Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi alisema kuwa anaunga mkono uamuzi wa kupiga marufuku maandamano hayo, akitolea mfano vurugu zilizotokea mwishoni mwa wiki iliyopita. Akizungumza katika mahojiano yake ya kwanza tangu achukue hatamu za uongozi mapema mwaka huu, Tshisekedi alikiambia chombo kimoja cha habari cha Ufaransa kwamba ana hisi kuna baadhi ya watu wanaojichanganya na kushindwa kutofautisha kati ya demokrasia na uasi.

Wiki iliyopita, wakati kiongozi wa upinzani Jean-Pierre Bemba aliporejea nchini, polisi walilazimika kutumia gesi ya machozi dhidi ya waandamanaji ambao walilushambulia msafara wa Bemba kwa mawe.

Maandamano ya Jumapili yaliitishwa na Bemba na Fayulu, ambao wanasisitiza kuwa wameibiwa ushindi wao katika uchaguzi wa Rais uliofanyika Desemba 30 katika nchi hiyo iliyokuwa zamani koloni la Ubelgiji.

Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi
Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix TshisekediPicha: Presidence RDC/G. Kusema

Muungano wa vyama vya LAMUKA ulisema mwishoni mwa juma kwamba utaendelea mbele na maandamano ya kupinga uamuzi wa mahakama ya katiba wa kufuta  uchaguzi wa wabunge 20 wa upinzani. Mkuu wa polisi wa Kinshasa Sylvano Kasongo alikuwa ameonya kuwa mikusanyiko yoyote ya watu zaidi ya 10 leo Jumapili itatawanywa.

Fayulu anamlaumu Rais Tshisekedi, ambaye yeye mwenyewe ni kiongozi wa upinzani wa muda mrefu, kwa kuwa kibaraka wa Rais wa zamani Joseph Kabila. Muunganao wa vyama vinavyoongozwa na Kabila una viti vingi zaidi bungeni.

ChanzoL:/AFP