Pongezi kwa Learning by Ear
7 Juni 2011Mchezo wa Redio wa Learning by Ear kuhusu " Ushiriki katika siasa " ulishinda tuzo ya shirikisho la kimataifa la vyombo vya habari, AIB (Association for International Broadcasting Award) mwaka 2009 katika kitengo cha Ubunifu bora wa Mchezo wa redio".
Waamuzi waliridhishwa na ubunifu wa hali ya juu na hali halisi ilivyoelezewa kupitia mchezo huo. Mchezo huo uliandikwa na mwandishi maarufu wa michezo, na msanii Chrispin Mwakideu kutoka nchini Kenya. Mchezo huo unaelezea changamoto wanazopitia vijana barani Afrika na jinsi wanavyokabiliana na changamoto hizo. Kadhalika mwezi Novemba mwaka 2010, mchezo wa redio kwa jina "Hapo zamani za kale – Historia ya Afrika’’ pia ukachaguliwa kushindania tuzo hiyo.
Mchezo kuhusu "Wanawake na wasichana barani Afrika" watuzwa nchini Ureno
Mwezi Mei mwaka 2009, mchezo wa redio wa Learning by Ear kuhusu "Wanawake na wasichana barani Afrika - maisha magumu" ulishinda tuzo ya mwandishi bora wa Ureno ya Prémio Paridade mjini Lisbon. Tuzo hiyo ilitolewa rasmi na kamishna wa tume ya kutetea haki za kiraia na usawa wa kijinsia wa Ureno. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa shirika la habari la kimataifa kutunukiwa tuzo hiyo ya Prémio Paridade. "Mfululizo wa mchezo huu wa Deutsche Welle ni mfano bora wa jinsi ujumbe unaoweza kubadili fikra unavyoweza kuenezwa kupitia vyombo vya habari kuhakikisha wanawake na wanaume wanapata nafasi sawa," lilisema jopo la waamuzi.
Kwa niaba ya timu nzima ya mradi wa Noa Bongo, tuzo hiyo ilipokewa na mkuu wa idhaa ya Kireno ya Deutsche Welle, Johannes Beck, Zainab Aziz, mwandishi wa mchezo huo kutoka nchini Kenya na mkuu wa idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle, Andrea Schmidt, mratibu wa mchezo huo.
Learning by Ear, jungu la ubunifu katika nchi ya mawazo mapya
Mradi wa Noa Bongo pia ulipata umaarufu na kutambulikana nchini Ujerumani. Mwaka wa 2010, Learning by Ear iliteuliwa kuwa "Mahali palipochaguliwa" kwenye shindano la kitaifa kwa jina "365 Places in the Land of Ideas" yaani Maeneo 365 katika nchi yenye mawazo mapya. Jopo la waamuzi lilitambua kuwa vipindi vya Noa Bongo vinaiwakilisha Ujerumani kama nchi ya mawazo mapya: yanazingatia siku za usoni, yenye ubunifu na mapana. Jopo hilo lilisema lina matumaini kuwa mradi huu ungewatia moyo watu wengine.
Tuzo hiyo ilitolewa Septemba 2010 kwenye ghafla ya kufana iliyoandaliwa katika makao makuu ya Deutsche Welle mjini Bonn. Wakati wa ghafla hiyo mkurugenzi mkuu wa Deutsche Welle, Erik Betterman, aliipokea tuzo hiyo kwa niaba ya kikosi kizima cha mradi wa Noa Bongo. Wakati wa sherehe hiyo wanafunzi kutoka shule ya upili ya Friedrich-Ebert mjini Bonn, chini ya uongozi wa msaanii na mwandishi mashuhuri wa michezo ya kuigiza kutoka nchini Kenya, Chrispin Mwakideu, waliigiza baadhi ya sehemu za michezo ya Noa.
Michezo ya Noa Bongo hutayarishwa katika lugha sita na kupeperushwa hewani katika mataifa 50 barani Afrika. Kufikia sasa zaidi ya makala na michezo 27 imetayarishwa na Deutsche Welle tangu mwaka 2008. Mradi wa Noa Bongo hutekeleza jukumu kubwa muhimu katika maisha ya vijana barani Afrika, kwa kuwatayarishia michezo ya redio na makala kuhusu mada mbalimbali, kuanzia masuala ya kisiasa, na kijamii, hadi kiuchumi, kiafya na kimazingira.