1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PRETORIA.China na Afrika Kusini zatia saini makubaliano ya kibiashara

7 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCUF

Rais Hu Jintao wa China anaezuru bara la Afrika leo ametia saini makubaliano ya kibiashara na rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini.

Hu Jintao ambae yuko katika ziara ya siku nane barani Afrika amesema kwamba uhusiano unaoendelea kuimarika kati ya China na nchi za Afrika utaleta mafanikio makubwa kwa pande zote.

Amemueleza rais Thabo Mbeki kwamba angetaka uhusiano wa karibu wa kisiasa baina ya nchi hizo mbili.

Pia ameongeza kusema kuwa China ikiwa ni mwanachama wa kudumu katika baraza la usalama la umoja wa mataifa itafurahika kuona bara la Afrika likiwa na uwakilishi madhubuti katika baraza hilo la usalama.

Ziara ya rais Hu Jintao imekosolewa kuwa ina lengo la kutimiza uchu wake wa mali asili na mafuta katika bara la Afrika na wakati huo huo kupeleka bidhaa zake za bei rahisi barani humo.

Rais Hu Jintao anatarajiwa kutoa hotuba yake rasmi hapo kesho.