1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin atoa mwito wa kuahirisha kura ya maoni,Hague azikaanga mbuyu

Abdu Said Mtullya7 Mei 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague amesema Urusi inawatumia wapiganaji wa siri na inaendesha Propaganda ya kiwango kikubwa kwa lengo la kuzuia kufanyika uchaguzi wa Rais nchini Ukraine

https://p.dw.com/p/1BvJ6
Rais Vladimir Putin wa Urusi akutana na Mwenyekiti wa OSCE Didier Burkhalter mjini Moscow
Rais Vladimir Putin wa Urusi akutana na Mwenyekiti wa OSCE Didier Burkhalter mjini MoscowPicha: Reuters

Waziri Hague ameyasema hayo katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev, wakati Rais Vladimir Putin wa Urusi amewataka watu wanaotaka kujitenga waziahirishe kura za maoni walizozipanga kuzifanya mwishoni mwa wiki.

Waziri Hague amesema ikiwa Urusi itafanikiwa katika mipango yake,hilo litakuwa pigo kubwa kwa demokrasia. Waziri huyo wa Uingereza pia ameilaumu Urusi kwa kufanya njama za kuandaliwa kura ya maoni mashariki mwa Ukraine mwishoni mwa wiki hii kwa lengo la kuuhujumu uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 25 ya mwezi huu nchini Ukraine.

"Wanajeshi maalumu wa Urusi"

Waziri Hague aliwaambia waandishi habari baada ya kukutana na viongozi wa Ukraine kwamba hakuna shaka hata kidogo kwamba serikali ya Urusi inachochea mgogoro na inafanya uchokozi mashariki mwa Ukraine.Waziri wa Uingereza amesema kwamba majeshi ya serikali ya Ukraine hayapambani tu na watu wenye nasaba ya kirusi wanaotaka kujitenga, bali pia wanapigana na majeshi maalumu ya Urusi, kama yale yaliyopelekwa katika jimbo la Krimea .

Putin ataka kura ya maoni iahirishwe

Wakati huo huo Rais Vladimir Putin wa Urusi amewataka watu wa kusini mashariki mwa Ukraine wanaotaka kujitenga wazihairishe kura za maoni walizopanga kuzifanya mwishoni mwa wiki.

Rais Putin amewaomba wawakilishi wa majimbo ya kusini mashariki mwa Ukraine wazihairishe kura za maoni ili kuweza kuyaleta mazingira mazuri ya kufanyika mazungumzo. Rais Putin ametoa mwito huo baada ya kukutana, mjini Moscow na mwenyekiti wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya ,OSCE Didier Burkhalter, ambae pia ni Rais wa Uswisi.

Kwa kura hizo za maoni wanaharakati wanaoiunga mkono Urusi wa kusini mashariki mwa Ukraine wanataka kuamua juu ya kujipa mamlaka makubwa zaidi ya kujitawala au kuamua juu ya kujitenga na serikali kuu ya Ukraine.

Hata hivyo wanaharakati wa mji wa Donetsk wamesema watautafakari mwito uliotolewa na Rais Putin kutokana na kumheshimu sana kiongozi huyo wa Urusi.

Rais Putin pia amesema kuacha kutumia nguvu ni sharti la lazima kwa ajili ya kufanyika uchaguzi wa rais nchini Ukraine hapo tarehe 25.

Rais wa Urusi amesema anataka kuletwa suluhisho la haraka, kwa kadri itakavyowezekana,katika mgogoro wa Ukraine,litakaloyazingatia maslahi ya watu wote wa Ukraine.

Mwandishi:Mtullya Abdu/afpe,

Mhariri:Mohammed Abdul-rahman