PYONGYANG: Korea Kaskazini yadai Marekani imeifuta kutoka orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi
3 Septemba 2007Korea Kaskazini inasema Marekani imekubali kuiondoa kutoka kwa orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi.
Msemaji wa wizara ya mashauri ya kigeni ya Korea Kaskazini amesema Marekani imekubali pia kuondoa vikwazo vilivyowekwa kuhusiana na sheria ya kufanya biashara na nchi hasimu, lakini haya bado hayajathibitishwa na Marekani.
Korea Kaskazini iliwasilisha ombi la kutaka kufutwa kutoka kwa orodha ya Marekani ya nchi zinazodhamini ugaidi ili kuipa ushawishi mkubwa zaidi ulimwenguni. Katika mkutano kati ya Marekani na Korea Kaskazini uliofanyika mwishoni mwa juma mjini Geneva Uswisi, mpatanishi wa Marekani katika mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini, Christopher Hill, alisema serikali ya Pyongyang imekubali kumaliza mpango wake wa nyuklia kufikia mwishoni mwa mwaka huu.
Korea Kusini imeikaribisha hatua ya Korea Kaskazini kukubali kumaliza mpango wake wa nyuklia, lakini ikaonya kuwa mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika kati ya pande sita huenda yakawa magumu.