PYONGYANG: Shutuma zinazoenezwa hupotoza maoni ya umma
27 Januari 2007Korea ya Kaskazini inakanusha madai kuwa inashirikiana na Iran katika mradi wa kinyuklia. Shirika la habari la Korea ya Kaskazini KCNA limemnukulu msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje akisema kuwa vyombo vya habari vya nchi za magharibi,vinaeneza shutuma hizo ili kupotoza maoni ya umma.Baada ya serikali ya Pyongyang kufanya jeribio lake la kwanza la nyuklia Oktoba mwaka jana,Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kuiwekea Korea ya Kaskazini vikwazo vinavyozuia kuipatia zana za kijeshi na silaha.Baraza la Usalama pia kwa kauli moja mwaka jana,lilipiga kura kuweka vikwazo dhidi ya Iran,kuhusika na biashara ya zana na teknolojia ya kinyuklia.Lengo ni kujaribu kuzuia kazi za kurutubisha madini ya uranium ambayo huweza kutumiwa kutengeneza silaha za nyuklia.